HabariNews

Sodo Zitolewe BURE kuimarisha Mabanati Kimasomo

Serikali imetakiwa kuweka mikakati endelevu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa sodo miongoni mwa wasichana nchini ili kuwawezesha kuendeleza shughuli zao za masomo bila pingamizi.

Akizungumza katika zoezi la kupeana msaada wa sodo katika shule ya msingi ya Central mjini Mombasa, seneta maalum Miraj Abdulahi alieleza haja ya wanafunzi wa kike kupewa sodo za bure kama njia ya kuhakikisha wanasalia shuleni na kufanikisha ndoto zao za kielimu.

Miraj alitaja changamoto hiyo kama sababu mojawapo zinazochangia matokeo duni katika mitihani ya kitaifa miongoni mwa wanafunzi wa kike katika kaunti ya Mombasa.

Ni jukumu letu sisi pia kuweza kuendeleza pale ambapo wao wametuachia, ili tuone mtoto wakike hafai wala hapaswi kukosa shule ati kwa sababu hana sodo ya kumueka yeye darasani. Kwa tamu moja mtoto huyu anaingia ndani ya mwezi wake siku kumu na mbili, kuonesha ya kwamba ni watoto wengi wa kike wanakosa kufika darasani lakini mwishowe walimu wanaweza kuwaeka daraja moja na wale wenzao wa kiume kwa alama zile zile ambapo hawa wa kike wanakosa shule.” Alisema

Swala hilo liliungwa mkono na baadhi ya viongozi walioandamana naye akiwemo Mkurugenzi wa Elimu kaunti ya Mombasa James Mureithi aliyesisitiza kuwa hatua hiyo ni yenye manufaa katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha kuwa inaondosha baadhi ya vikwazo vinavyoikumba.

Wakati huo huo Naibu Kamishna wa Polisi kaunti ya Mombasa Ronald Mwiwawi aliwahakikishia wanafunzi usalama wao akiahidi kupambana na makundi ya uhalifu yanayowahangaisha wakaazi eneo hili.

Ni mikakati mizuri ambayo inaonyesha kazi safi inayotekelezwa na serikali yetu, na itawezesha wasichana wetu kusalia shuleni. Kama asasi za usalama tutahakikisha usalama mjini unapewa kipombele kuhakikisha kwamba hawa wasichana wanaweza kufika shule salama na kurejea makwao salama , tutalemaza magenge yote ya uhalifu yaliyokuwepo Mombasa”  Mwiwawi alisisitiza.