Uncategorized

Maonyesho ya Kilimo ya Mombasa: Serikali Ikiahidi kupiga jeki Wakulima

Serikali imeahidi kuwapiga jeki wakulima kwa kuwapa mgao wa fedha zaidi ili kuendelea kuimarisha kilimo hapa nchini.

Akizungumza Septemba 8, 2023 wakati wa kufungua rasmi Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Mombasa katika Uwanja wa Mkomani, Naibu rais Rigathi Gachagua alisema kuwa wakulima wametengewa takribani shilingi bilioni 3.7.

Gachagua alisifia maonyesho hayo kwa kutoa nafasi kwa wakazi wa Mombasa, Pwani na kote nchini kwa jumla ili kuonyesha bidhaa na mazao pamoja na kujifunza mengi.

Serikali imetenga shilingi bilioni 3.7 kuimarisha miradi ya kilimo na kuwapiga jeki wakulima, na shilingi bilioni 1.5 kwa mpango wa uboreshaji kilimo cha ufugaji wa mifugo nchi,” alisema Gachagua.

Vile vile naibu rais aliwataka Wakenya kukumbatia kilimo zaidi ili kupunguza gharama ya maisha akisisitiza kuwa kilimo ndicho uti wa mgongo wa taifa hili na sekta mwafaka ya kuimarisha taifa kukabiliana na njaa.

Wageni waheshimiwa, Mabibi na mabwana ni uamuzi sahihi kabisa kuwekeza katika kilimo kumarisha na kufufua uchumi wetu wa Kenya. Kupunguza gharama ya maisha na kushusha bei ya vyakula lazima tukumbatie kilimo. Niwapongeze Wadau wa Shirika la Kilimo Nchini, wakulima wenye bidii washikadau na Wizara ya Kilimo kwa kusimama pamoja kufanikisha maonyesho haya,” aliongeza.

Hata hivyo Gachagua  alidokeza kuwa serikali ina mpango wa kuimarisha kilimo cha zao la mnazi na kuahidi kupeana kwa wakulima mbegu za mmea huo.

BY EDITORIAL DESK