HabariNewsSiasa

Gharama ya Maisha? Punguza idadi ya Kaunti na Wabunge!’ Asema Mwanasheria Mkuu wa zamani

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Githu Muigai, ametoa pendekezo la kupunguza idadi ya kaunti na maeneo bunge ili kupunguza matumizi ya fedha ya serikali ya kila mwaka

Akizungumza mbele ya kamati ya Mazungumzo ya maridhiano katika ukumbi wa Bomas alikofika kutoa mapendekezo yake siku ya Alhamisi Septemba 28, Muigai alisema idadi ya maeneo bunge na pia idadi ya kaunti nchini inafaa kupunguzwa ili kudhibiti matumizi zaidi ya fedha za serikali kila mwaka.

“Tuna watu wengi bungeni, tuna mabunge mengi na kaunti. Zinatugharimu pesa nyingi sana. Punguza mabunge yawe kama 100 na kuwe na mbunge mmoja wa kiume mmoja wa kike kote,” alisema.

Mwanasheria mkuu huyo wa zamani aidha alipendekeza nyadhifa za kisiasa zipunguzwe akilenga wadhifa wa mwakilishi wa kike kila kaunti ambao amependekeza utupiliwe mbali.

Wakili huyo maarufu aliongeza kuwa sheria ya thuluthi tatu ya jinsia inapaswa kuondolewa na badala yake kuwe na uwakilshi wa sawa wa aslimia 50/50 ujumuishwe serikalini.

“Tunahitaji kuondoa kiti cha Mwakilishi wa Wanawake, tuunde nafasi mbili katika bunge. Tutafikia asilimia 50, na itakuwa rahisi,” alisema Muigai.

Na iwapo angetaka uchaguzi mkuu wa Agosti 9 hufanyiwe ukaguzi, Muigai amesema hilo halifai kufanyika kwani litakuwa  jaribio la kudunisha mamlaka ya mahakama ya upeo.

“Hivi kuna ulazima gani turudi nyuma kweli tujiulize kilichotokea katika Uchaguzi wa 2022? Rai yangu kiukweli nasema si muhimu, kwa nini haisaidi na si muhimu? Kwa sababu tunafungua tena kurudisha suala ambalo limeamuliwa kwa uamuzi wa mwisho na mahakama. Changamoto ya kufungua upya masuala yaliyoamuliwa na mahakama ni kuwa unaunda uwezekano wa kushusha na uaminifu kwa Idara hiyo unaweza ukavunjika,” alisema Muigai.

Ikumbukwe kamati ya mazungumzo yenye wanachama kumi inajadili masuala ya washikadau tofauti ili kutatua migogoro ya kisiasa na kiuchumi ambayo imedumu kwa muda mrefu.

BY MJOMBA RASHID