HabariLifestyleNews

Mikakati mipya! Serikali yaapa kutumia nguvu zote kukabiliana na Ugaidi Pwani

Serikali ya Kitaifa kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani nchini imewahakikishia wakazi wa Pwani, Kaskazini Mashariki na Wakenya kwa ujumla kwamba inaendelea kutumia nguvu zote kukabiliana na ugaidi.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, katibu wa kudumu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt. Raymond Omollo amesema mikakati hiyo ikiwemo vikao na wakuu wa usalama inalenga kukomesha visa vya ugaidi akiongeza serikali imejitolea kufanya kila iwezalo ili kuhakikisha imefanikiwa kukomesha ugaidi.

“Kuna mikakati mingi tumeweka kushughuliokia suala la ugaidi, kwanza kuwasiliana na kushirkiana na watu wote serikalini na wananchi wenyewe pamoja na viongozi, hili jambo tunashughlikia kila sehemu sana sana hapa Pwani na Kaskazini Mashariki. Tunegemea suala la Polisi jamii na kuhusisha jamii na tutafanya njia zote kupambana nah ii,” alisema Omollo.

Kadhalika Dkt Omollo amezitaka jamii zilizopoteza wapendwa wao katika msitu wa Shakahola kwa sababu ya mafundisho ya kupotosha kuwa na uvumilivu akisema kwa muda wa mwezi mmoja na nusu ujao shughuli ya DNA inatarajiwa kukamilika na kisha serikali itatoa mwelekeo.

Katibu huyo alikuwa ameandamana na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja miongoni wa washikadau wengine katika idara ya usalama nchini.

Kanja amewataka wakazi katika eneo hilo kushirikiana na maafisa wa usalama ili kukabiliana na masuala ya utovu wa usalama, huku akiwahakikishia wakenya kuwa ugaidi utakomeshwa ipasavyo hapa nchini.

“Nataka kuhimiza jamii ya eneo hili waendelee kufanya kazi na polisi ili masuala yanayowaathiri ya usalama yanashughulikiwa na makamanda hawa wako hapa,” alisema Kanja.

Itakumbukwa kuwa viongozi wa ngazi za juu serikalini  kupitia  Wizara ya Usalama wa Ndani na Wizara ya Ulinzi wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara kaunti ya Lamu wakiweka mikakati kadhaa ya kupambana na magaidi wanaohaingaisha wakazi wa Lamu na viunga vyake.

BY MJOMBA RASHID