HabariNews

Fungua sava! Amos Wako atoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa

Aliyekuwa Mwanasheria mkuu nchini Amos Wako ameeleza haja ya kufunguliwa kwa sava za tume ya uchaguzi IEBC ili kurekebisha makosa ambayo huenda yalifanyika wakati wa uchaguzi.

Akiwa mbele Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa kwenye ukumbi wa Bomas, mnamo Jumatatu Oktoba 2, Wako alisema kunapaswa kufanywa ukaguzi wa matokeo ya kura za urais kila baada ya uchaguzi ili kurekebisha matatizo ambayo yalikumba uchaguzi uliopita.

“Ukaguzi ni kama uchunguzi wa maiti ambao hauwezi kurejesha maiti hai ila itatoa sababu iliyopelekea kifo. Na hivyo basi tunataka kujua katika ukaguzi huu wa matokeo tujue na tutambue matatizo, udhaifu na makosa yaliyotokea na ambayo tunaweza tukayarekebisha kabla uchaguzi mwingine ujao.” Alisema.

Wako vile vile alisema hatua hiyo itawahakikishia wakenya wapiga kura kuwa mchakato wa uchaguzi ulifanyika kwa njia huru na haki.

“Ukaguzi wa kisawasawa wa matokeo unapaswa kufanywa kabla uchaguzi mwingine. Kwanza ndio njia pekee tunaweza tukaimarisha mchakato wa uchaguzi na kujenga imani kwa wapigakura katika mchakato na taasisi ya kura,” alisema Wako.

Aidha Wako ambaye pia alikuwa seneta wa Busia alibaini kuwa kulingana na waangalizi wa uchaguzi wa mwaka 2022, shughuli nzima iliendeshwa kwa njia ua uwazi isipokuwa kutangazwa kwa matokeo ya urais.

“Waangalizi wengi wa matokeo waliangalia na kutambua kuwa kwa kawaida shughuli nzima ilikuwa sawa na ya haki kabisa na kuhesabu kura vituo ilikuwa ya haki. Shida inatokea kwenye kujumlisha na kutangaza matokeo.” Alisema

Kando na hayo Wako alipendekeza kubuniwa kwa hazina ya kupunguza umasikini ili kushughulikia mahitaji ya kiuchumi ya wakenya waaoishi katika mitaa ya mabanda.

Wako alitaja kuwa kundi la watu linaloishi katika vitongoji duni au mitaa ya mabanda limetengwa, pamoja na changamoto za kiuchumi na umasikini uliokithiri ambao umeathiri Wakenya wengi unasababisha kuenea kwa mitaa hiyo sio tu viungani mwa miji mikubwa bali pia katika maeneo ya mashambani.

BY MJOMBA RASHID