Serikali ya kaunti ya Kilifi imepewa makataa ya siku 30 kuafikia makubaliano ya mkataba baina yao na madaktari.
Mwenyekiti wa Muungano wa Madaktari eneo la Pwani KMPDU, Dkt. Niko Gichama amelalamikia hatua ya kuhangaishwa katika mchakato wa kuafiki waliokubaliana katika mkataba wa pamoja na serikali ya kaunti hiyo.
“Tumekuwa tukijaribu tukiongea nao muda kutoka hii serikali mpya ya ugatuzi kilifi iingie, tumekuwa na mikutano kadhaa lakini wanatuzungusha tunapelekwa huku na kule. Hatuelewi!” Alisema
Gichama alisema kuwa madaktari walioajiriwa na serikali katika eneo hilo wanapitia changamoto ya malipo duni, akiitaka kaunti kuwaongezewa mshahara ili kumudu kikamilifu mahitaji yao ya kimsingi ikizingatiwa kuwa matozo ya ushuru yameongezeka na gharama ya maisha imepanda.
“Tunamuomba gavana wetu Mung’aro aingilie kati, awasukume madaktari wetu wa Kilifi wapate haki yao na tumewapa siku 30 waamue vile wanataka tuende sisi madaktari wa sababu tumekuwa wavumilivu sana lakini hali inatuumiza sana,” alisema Gichama.
Daphne Akoth Mwakilishi wa madaktari kaunti ya Mombasa aliunga mkono kilio cha madaktari wa Kilifi akisisitiza kuwa ni muhimu kuangazia maslahi ya madaktari kwa manufaa ya mwananchi.
“Kuna kaunti zimepiga hatua katika kutekeleza mkataba wa makubaliano CBAs, na kuna kaunti zingine hazijatekeleza hatua yoyote na inafanya madaktari wanakufa moyo na zinachangia mfadhaiko na wengine kuacha kazi. Tungeomba watekeleze masuala hayo hatungependa madaktari wagome waache kazi kwa sababu ya afya ya Kilifi na wakenya wote na tukiacha kazi wananchi ndio wanaumia,” alisema Dkt. Daphne.
Daphne hata hivyo alisisitiza kuwa serikali inapaswa kutekeleza majukumu yake pasi na kushurutishwa na mtu yeyote ili kufanikisha maendeleo nchini.