Jopokazi la mageuzi ya polisi nchini limewasilisha ripoti yake kwa rais William Ruto.
Jopokazi hilo linaloongozwa na mwenyekiti wake aliyekuwa Jaji Mkuu nchini David Maraga limewasilisha ripoti yake kipindekeza mageuzi kadhaa kutekelezwa.
Ripoti yake Maraga imependekeza Idara za Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Huduma za Magereza na Huduma ya Vijana ya Taifa NYS kuhamishiwa kwa Sekta ya Usalama kwa kulingana na marupurupu na vigezo vya huduma.
Akiongea baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo mnamo siku ya Jumatano, Rais Ruto ambaye alikubali mapendekezo matatu ya ripoti hiyo alisema kwa namna hiyo maafisa katika vitengo hivyo watapata malipo na marupurupu yao kwa vigezo vingine vya huduma kwa mujibu wa kazi wanazofanya.
Alisema aidha kutawezesha maafisa wenye tajriba na chapakazi kuajiriwa kuhudumu katika idara ya polisi nchini.
“Kwa namna hii maafisa katika vitengo hivyo vitatu vya huduma watapata malipo kwa kuzngatia vigezo vya huduma, na kuelekea mbele hasa kipindi hiki cha utovu wa usalama na uhalifu kuongezeka mageuzi haya yatavutia maafisa wengi wazoefu na wenye tajriba katika kazi hii,” alisema Ruto.
Ripoti hiyo inaangazia kutekelezwa kwa sera ya uhamisho ya kitengo cha Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwamba hakuna afisa atakayesalia katika kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitatu.
Akikubaliana na pendekezo hilo la ripoti rais Ruto alilitaja kuwa pendekezo mwafaka na kwamba hakuna afisa atakayepandishwa cheo kwa kuhudumu katika kituo kimoja pekee.
“Kuendelea mbele haitawezekana kwa afisa wa polisi kupandishwa cheo ikiwa alihudumu katika kituo kimoja pekee,” alisema rais.
Vile rais ametoa hakikisho kuwa serikali yake imejitolea kuimarisha huduma za idara ya polisi huku akitangaza kuwa Jopokazi hilo litatoa ripoti yake kamili nay a mwisho katika muda wa mwezi mmoja.
BY MJOMBA RASHID