HabariNews

Siku ya Mtoto wa Kike Duniani: Jamii Pwani yalaumiwa kuendekeza dhulma dhidi yao

Na huku taifa likiadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, Wazazi na wadau mbalimbali eneo la Pwani wamelaumiwa kuendekeza dhulma za Mtoto wa kike bila kuchukua jukumu la kumlinda.

Kulingana na Afisa wa masuala ya jinsia na haki za wanawake kutoka shirika la Haki Afrika Salma Hemed, kunyanyasika kwa mtoto wa kike ni kutokana na jamii kutowajibika kikamilifu katika kumlinda mtoto wa kike.

Akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, iliyoadhimishwa Oktoba 11, Salma alisema kuna haja ya maswala ya kumlinda mtoto wa kike kuangaziwa kwa undani zaidi ili kumlinda na changamaoto ambazo zinaweza kumkumba.

Tunaadhimisha siku hii kwa masikitiko sana, bado kuna haja ya kuangazia mambo ya mtoto wa kike, mimba za mapema hasa Kilifi na maeneo mengine ya Pwani kesi zimekithiri kwa kiwango cha juu, kila siku tunaangazia vipi watoto wadogo wanapata mimba,” alisema.

Aidha Bi. Salma alisema mtoto wa kike hujipata kwenye hali ya utata hasa kwa wale wanaorandaranda barabarani, akiirai serikali kuchukua jukumu la kuwatafutia makao ya watoto hao ili waweze kuwa kama watoto wengine.

Watoto wa kurandaranda barabarani wako wengi sana na wanapitia madhila mengi sana wanapokuwa barabarani, tunachokiomba serikali ni iangalie vipi itachukua majukumu ya kuondoa watoto haw ana familia zao iangaliwa wapi itawapa nafasi ili waweze kuwa kama watoto wengine, kuwe na vituo vya kuwanusuru na kuwahifadhi hawa,” alisema Bi. Salma.

Sophie Kadzo Kombe ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Hazina ya Ustawishaji Wanawake kaunti ya Kilifi alitaja suala la mimba za utotoni miongoni mwa wasichana kama mojawapo ya changamoto kuu zinazokumba kaunti hiyo.

Alihimiza ushirikiano baina ya washikadau mbalimbali wakiwemo wazazi, wazee wa mitaa na asasi za usalama katika kupambana na swala hilo.

Hapa Kilifi county changamoto za mtoto wa kike ni nyingi sana, Mtoto hakuzwi na mzazi mmoja, tunahitaji jamii nzima ijumuike ishirikiane pamoja katika malezi. Jamii, wazee wa mitaa sote tukishikana pamoja tutakuwa na watoto wema, wabunifu na wenye afya na kuifaa jamii,” alisema.

Kwa upande wake Christine Rashid kutoka Shirika la Strategic Community Development alieleza haja ya kumwezesha na kumwelimisha mtoto wa kike kuhusu haki zao sawia na kumlinda dhidi ya mila potofu na dhulma za kijinsia.

Kuna haja zaidi kumwezesha msichana, maana hizi mimba za mapema zinatoka wapi kama hawa wasichana wangekuwa wameelimishwa? Kuna wasichana bado wanakeketwa Kenya hii, kwa nini? Kuna wale wanaoleka kwenye ndoa za mapema na kwenye ndoa hizo hudhulimiwa kijinsia kwa hivyo bado kuna kazi ya kufanya ili kuondoa haya,” asliema Bi. Christine.

Siku ya kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa kila tarehe 11 mwezi Oktoba, huku kauli mbiu ya mwaka huu 2023 ikiwa ‘Kuwekeza katika haki za wasichana; Uongozi wetu, Ustawi wetu.’

BY MJOMBA RASHID