HabariNews

Shirika la Muhuri Latetea Haki kwa Mackenzie na Wenziwe

Shirika la kutetea Haki za Binadamu MUHURI, limetaka mshukiwa mkuu wa mauaji ya halaiki ya shakahola, Paul Mackenzie na washukiwa wenza kuachiliwa maramoja iwapo serikali imekosa ushahidi .

Akizungumza na Sauti ya Pwani afisa wa dharura wa shirika hilo Francis Auma alisikitishwa kuona haki za Mackenzie na washukiwa wenzake zinakiukwa kiholela na asasi za haki nchini.

Kulingana na Auma, Mackenzie pamoja na washukiwa wenzake wanafaa kuachiliwa iwapo ushahidi dhidi yao haupo au wafunguliwe mashtaka iwapo wamepatikana na kesi ya kujibu badala ya kuhangaishwa bila hatua mwafaka kufuatiwa.

‘‘Sisi kama watetezi wa haki za ki binadamu katika nchi ya kenya tunaona kuwa suala la Mackenzie kufikishwa kizimbani na hawamfungulii mashtaka rasmi ili aanze kesi, ni jambo la kusikitisha mno.Yeye na wanzake walioshikwa, tunataka haraka iwezekavyo Mackenzie na wenzake wafikishwe kortini ili waanze kesi yao mara moja.  Na iwapo wanaowachunguza watakuwa bado hawako tayari basi wawachilie na wakati watakuwa tayari watamshika na kumwelekeza kortini’’ Alisema

Shirika hilo lilishutumu na kukashifu idara ya upelelezi wa jinai DCI kwa kuzembea kutafuta ushahidi dhidi ya washukiwa hao wa mauaji ya shakahola likisema licha ya asasi za upelelezi kukita kambi shakahola kazi yao imekuwa duni na ya kutiliwa shaka.

Imechukua muda mrefu, Ofisi ya mashataka ya umma (Dpp) imezembea ki kazi. Vilevile wachunguzi wa kesi hii kutoka Idara ya upelelezi wa jinai (DCI) inaonekana wamezembea. Na si jambo geni watu wengi wanapata shida hapa kenya kwa sababu ya kuzembea kwa taasisi ambazo zinafaa kuchunguza na kuhakikisha kuwa hata mshukiwa pia ako na haki kulingana na katiba. Haki yao ikicheleweshwa, basi inaumiza watu wengi. Meckenzie amekaa pale korokoroni, ila haki zake zimekiukwa.’’

Kwa upande wake Auma, mahakama  ilikiuka haki za washukiwa hao kutokana na hatua ya kuridhia ombi la idara ya DCI kutaka kupewa muda zaidi kufanya uchunguzi kesi ifikapo mahakamani.

Licha ya polisi kuomba muda mrefu wakisema wanataka muda wa kufanya uchunguzi, hili ni jambo la kikorofi. Na vilevile tunaona mahakama pia inaridhia ombi lao kila mara. Mahakama yatakikana isikubali kutumiwa vibaya  maana mahakama pia italaumiwa hapa. Kwa nini mahakama inazidi kuwapatia muda? Inalekea miezi zaidi ya mitano, Mackenzie bado kesi yake haijasikizwa mahakamani. Hili ni jambo mbaya sana na tunataka watu walizungumzie kwa kina na mapana.’’ Aliongezea

Mackenzie alitarajiwa kufika mbele ya kamati ya seneti inayochunguza mauaji ya shakahola kujitetea dhidi ya kesi inayomkabili mnamo Oktoba 13 ambapo alikataa kufika .

 BY ISAIAH MUTHENGI