Sekta ya usanii kaunti ya Mombasa imetajwa kunawiri kutokana na uzinduzi was sera zinazotoa mwongozo wa utengenezaji wa filamu.
Mwenyekiti wa kundi la vijana la Alpha and Omega Victor Odongo alikiri kuwa sekta hiyo ilikuwa bila mwelekeo hapo awali jambo analolitaja kubadilika hivi karibuni baada ya idara hiyo kuongozwa na sera zitakazoistawisha sio tu Mombasa bali Pwani kwa ujumla.
Kulingana na Odongo, licha ya sekta hiyo kuwa na sera zinazotoa mwongozo kwa wasanii bado kuna changamoto ya kimapato inayowakumba wasanii hasa wale wa mashinani. Odongo alitaka sera hizo kutumiwa kwa wasanii wa mashinani ili kutoa mafunzo zaidi.
“Sekta ya usanii Mombasa inaenda ikifufuka, ilikuwa iko ndivyo sivyo lakini saii wanajaribu sana.Mombasa film policy itakuwa inaongoza wasanii wote wenye wako Mombasa na ata Pwani kwa ujumla. Naona zikitiliwa maanani zitaweza kubadili sekta hii” alisema
Kwa upande wake Pauline Mutie mmoja miongoni mwa wasanii alibaini kuwa jamii kwa kiwango kidogo imekubali vijana kujihusisha na sanaa kutoka na ujio wa mtaala wa umilisi CBC akitaka wazazi na jamii kwa ujumla kutoa nafasi kwa vijana kujihusisha na usanii kama njia itakayowapatia ajira.
“Sasa hivi kidogo inaafadhali maana awali nikianza ilikuwa ni kama mzaha kusema mimi ni msanii ilikuwa ni mzaha.Lakini sasa kutokana na CBC Sanaa inaonekana kama njia ya kujipatia kipato.” Aliongezea Mutie