Ni afueni kwa wafanyabiashara nchini baada ya Katibu mkuu wa Wizara ya masuala ya ubaharia kutangaza kuafikiwa kupunguzwa kwa gharama ya usafirishaji wa bidhaa Bandarini.
Akizungumza na wanahabari kwenye jumba la KMA, Katibu Mkuu Idara ya masuala ya Ubaharia Geoffrey Kaithuko amewahakikishia wafanyabiashara kuwa katika siku zijazo watashuhudia punguzo la bei za kusafirisha mizigo kupitia usafiri wa majini.
Hatua hiyo ya wizara inajiri baada ya Rais William Ruto kukubaliana na ombi la washikadau wa Wizara hiyo ya kufanya biashara yenye ushindani kwa punguzo la ada wanazotozwa kupitia usafiri wa majini.
Katibu Mkuu wa idara ya Ubaharia Geofrey Kaithuko, aidha alibaini kwamba kama wizara watahakikisha kuwa Kenya itakuwa mshindani mkubwa wa biashara za bandarini kwa kupunguzwa kwa malipo ya usafirishaji bidhaa.
“Na tukiangazia taarifa hii ni kwa kupunguza gharama za usafirishaji kama ilivyoagizwa na Rais Ruto, nina raha nikisema kuwa hiki kikosi kimefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa imeangazia mapungufu ambayo yamekuwako kwa kuzingatia gharama, ili sisi kama taifa tuwe na ushindani katika sekta ya uchukuzi baharini,” alisema.
Hata hivyo mwenyekiti wa Mamlaka ya Baharini nchini, Kenya Maritime Authority, Hamisi Mwaguya ameongeza kuwa washikadau mbalimbali walihusishwa kikamilifu kwenye mchakato mzima wa kupungua kwa bei ya usafirishaji bidhaa na pia wanaunga mkono kikamilifu kupunguzwa kwa gharama hizo.
“Sisi kama mamlaka ya KMA, tutaunga mkono bidii za kupunguza gharama za kufanya biashara kwenye hili taifa na huu mchakato wote umekuwa wa huru kwa kuwashirikisha washikadau wote,” alisema Mwaguya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kitaifa wa shirika la kimataifa la Shehena na kuhifadhi maghala la Kenya, Roy Mwanthi aliwakikishia wafanyabiashara kuwa wateja wote watarudi nchini baada ya bandari ya Mombasa kurudishwa kuwa kitovu cha Afrika Mashariki na Kati baada ya utekelezwaji wa taarifa hiyo kutoka kwa Daresalaam.
“Taarifa hii ikitekelezwa Kenya itarejesha hadhi yakuwa kitovu cha Afrika Mashariki na Kati, miaka kadhaa iliyopita tulipoteza kwa Daresalam lakini hii ikitekelezwa wakenya wataona viwango vya juu kupitia kwa bandari ya Mombasa, na wateja walitoroka watarudi,” alisema Mwanthi.