HabariNews

Serikali Yanyooshewa kidole cha Lawama kwa Kusambaratika kwa Kaya

Serikali imenyoshewa kidole cha lawama na kudaiwa kuchangia kusambaratika kwa kaya kaunti ya Kilifi, kufuatia kutowajibika ipasavyo katika kutunza kaya hizo.

Mshirikishi mkuu wa kaya kaunti ya Kilifi Tsuma Nzai Kombe, alisema kuwakaya Fungo, Kauma,  Rabai, zilishuhudia ukataji wa miti kwa kiwango kikubwa jambo analodai kuchangiwa na utepetevu wa wazee wa kaya wanaosimamia kaya hizo.

Tsuma alihimiza kuwekwa kwa mikakati mipya kwa haraka ili kukabiliana na uharibifu wa miti inayopatikana katika maeneo hayo huku akiwataka wazee wanaosimamia kaya hizo kujiepusha kuingilia maswala ya siasa.

Aidha aliinyoshea kidole cha lawama serikali hasa wizara ya Jinsia, Utamaduni na turathi za kitaifa kwa kuchangia kuharibika kwa kaya, kutokana na kuwashawishi wazee kulegeza masharti na kukiuka miiko ya kaya.

Mshirikishi huyo hata hivyo aliutaka usimamizi wa utamaduni na turathi za kitaifa kuwachana na maswala ya kaya badala yake kutoa nafasi kwa shirika la kusimamia misitu nchini kusimamia kaya humu nchini.


BY ERICKSON KADZEHA