AfyaHabariNews

Tishio la Madaktari Kugoma Mwezi wa Likizo kaunti ya Kilifi

Madaktari katika kaunti ya Kilifi wametishia kugoma iwapo matakwa yao hayatatekelezwa ifikapo tarehe 19 mwezi wa Disemba, 2023.

Akihutubia waandishi wa habari katika hospitali ya rufaa kaunti ya Kilifi, katibu mkuu wa muungano wa madaktari nchini KMPDU tawi la ukanda wa pwani Ghalib Salim, alisema kuwa hatua hiyo inatokana na serikali ya kaunti ya Kilifi kufeli kushughulikia matakwa yao kwa muda mrefu.

Kulingana na Ghalib, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita madaktari kaunti ya Kilifi wamepandisha vyeo mara moja, huku akieleza kuwa madaktari hao hawajapewa nyongeza ya mishahara tangu mwaka wa 2014 tofauti na madaktari kutoka kaunti nyingine kama vile Mombasa na Taita Taveta.

Alitaja kuwa mgomo huo utaendelea na kujumuisha madaktari wote ukanda wa pwani, ili kushinikiza serikali za kaunti kuboresha maslahi yao.

“Tangu ugatuzi uanze, kwa miaka kumi ya gavana wa zamani madaktari kupandishwa vyeo kumefanyika mara moja, moja peke yake. Tena wote walitolewa kutoka kwa kiwango N hadi P. Na wale waliokuwa sio wataalam hawakupandishwa vyeo katika kiwango hicho cha N. Tumekaa vikao vingi ambavyo havijafanikiwa kuleta natija kwetu sisi madaktari, mtu anapata mshahara huo huo tangu mwaka 2014, wakati kila siku ushuru unaongezwa. Tumeanza na Kilifi, na tunatoa onyo kwa zile kaunti nyingine 5 ukanda wa pwani wajue, na tutapiga hili gurudumu kwa madaktari wote ukanda huu wa pwani wanaofanya kazi na kupitia hali ngumu.” alisema Salim.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa muungano huo tawi la ukanda wa pwani Daktari Niki Gichana, aliyesistiza kuwa ukosefu wa kutambulika kwa juhudi zao kazini pamoja serikali kukosa kuwapa nyongeza za mishahara kumefanya kazi yao kuwa ngumu, hii ikitokana na kuongezeka kwa gharama ya maisha iliyochangia madaktari wengi kukumbwa na matatizo ya msongo wa mawazo.

Niki alibaini kuwa iwapo serikali ya kaunti ya Kilifi haitashughulikia lalama hizo kufikia tarehe 19 mwezi huu wa Disemba, basi madaktari wote 122 kaunti ya Kilifi watalazimika kugoma.

“Kama mnavyokumbuka kuwa maisha mengi yaliweza kunusuriwa wakati wa tukio la kusikitisha la kimataifa la mauaji ya Shakahola, jambo tusilokumbuka ni kutotambulika kwa madaktari, hakukuwa na marupurupu, hakukuandaliwa gwaride la heshima kwa ajili ya madaktari, hatukupewa maua. Madaktari wetu wameendelea kupewa mikataba isiyostahili, tumejaribu kuishirikisha kwenye mazungumzo serikali ya kaunti ya Kilifi mara nyingi, tumejaribu kuwatafutia mikataba inayostahili madaktari wetu ambayo inafanyika kaunti nyingine kama vile Mombasa na Taita Taveta lakini hilo halijafanyika hapa kaunti ya Kilifi. Na kwa sasa hivi fununu za kuwepo kwa mgomo huu zinatokana na kutowajibika kwa utawala wa serikali ya kaunti ya Kilifi juu ya matakwa yetu hali inayopelekea kuanza kwa mgomo wetu tarehe 19 mwezi Disemba.” alisema Gichana.

BY ERICKSON KADZEHA