Waziri mwenye Mamlaka makuu nchini Musalia Mudavadi ametetea vikali serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya mfumo wake wa utozaji ushuru nchini.
Mudavadi amesisitiza kuwa mfumo wa serikali wa utozaji ushuru nchini sio wa ukandamizaji kama inavyoonekana na kudaiwa na wengi.
Alisema kuwa mikakati inayochukuliwa na serikali kupitia Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru KRA, inalenga kuimarisha vigezo vya ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi.
Aidha Mudavadi amesema kwa taifa kujikwamua kutoka hali ngumu iliyoko sasa, Wakenya ni sharti wakumbatie mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato yao wenyewe, huku akihakikisha kuwa serikali itaziba mwanya kwa kulinda makato yao.
“Hakuna nchi inayokua na kuwa imara kiuchumi bila kuwatoza ushuru raia wake. Serikali inapata mapato yake kuendesha shughuli zake kupitia kuomba mikopo pekee, suala linalopelekea madeni na kupitia kuwatoza ushuru wananchi wake. Hata katika mataifa yaliyoendelea hakuna anayefurahia kulipa ushuru lakini inasalia kuwa kujumu na kigezo cha kuisimamisha nchi imara,” alisema Mudavadi.
Wakati uo huo Waziri huyo mwenye mamlaka makuu aaliendelea kutetea hatua ya serikali ya Kenya Kwanza kuchukua mikopo kutoka kwa Shirika la fedha duniani, IMF na Benki ya Dunia.
Mudavadi alibaini kuwa Kenya ni mwanachama wa mashirika hayo ambayo kulingana naye hutoa mkopo wenye riba ya kiwango cha chini zaidi.
Mudavadi aidha alieleza kuwa ahadi ya serikali kwamba haitakopa fedha ilimaanisha kuwa haitakuwa ikikopa kutoka kwa mataifa ya nje bali kwa Mashirika ya fedha duniani kama IMF na Benki ya Dunia.
“Watu wakisema mbona serikali inakopa na walitwambia hatukopi lakini wanakopa kwa IMF, nataka wakenya wafamu kwamba Kenya ni wanachama wa benki ye dunia na tunapata mkopo wa IMF na Benki ya dunia japo kwa kiwango cha chini na tunapewa muda wa miaka 30 kulipa. Tunatumia nafasi hii kama wanachama ili tupate pesa ambazo hazitatuletea shida katika taifa letu.” Alisema Mudavadi
Kadhalika Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa masuala ya kigeni aliwaomba Wakenya kudumisha uzalendo na kuepuka kulisema vibaya taifa lao licha ya hali ngumu ya maisha akisisitiza kwamba serikali inaweka mikakati kabambe ili kuimarisha hali ya uchumi.
Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano na Idhaa moja hapa nchini.
BY OPCS