HabariKimataifaNews

Wapinzani nchini Congo waapa Kufanya Maandamano Kupinga Uchaguzi

Wagombea watano wa urais kutoka upande wa upinzani nchini Congo wamesema watafanya maandamano Desemba 27 mwaka huu mjini Kinshasa kupinga ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi mkuu uliomalizika.

Kwa mujibu wa Jean-Marc Kabunda, mwakilishi wa mgombea Martin Fayulu, wanasiasa hao wamewasilisha barua kwa gavana wa jiji la Kinshasa siku ya Jumamosi.

Kabunda alisema barua hiyo inaelezea azma ya maandamano hayo ambayo ni ya kupinga ukiukwaji uliojitokeza wakati wa kupiga kura na kabla ya zoezi la kupiga kura na kuongezwa zoezi la kupiga kura kwa siku moja zaidi.

Mwakilishi wa mgombea Martin Fayulu alisema kasoro zilizotajwa kwenye barua hiyo ni za kutosha kuona kwamba mnamo Desemba 20, 2023, uchaguzi wa nchini Kongo ulikuwa wa udanganyifu.

Tume ya uchaguzi nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, CENI, imekiri kuchelewa kuanza shughuli za kupiga kura mnamo Desemba 20 ambapo haikuwezekana kwa baadhi ya vituo kufunguliwa lakini tume hiyo ya uchaguzi imeyakanusha madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi huo kwa kuongeza muda wa kupiga kura.

Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili madarakani alikabiliana na wagombea wengine 18 wa upinzani kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Matokeo ya awali kutoka kwa maelfu ya wapiga kura wa jamii ya Wakongo walioko nje ya nchi yanaonyesha, Rais Felix Tshisekedi anaongoza dhidi ya wapinzani wake.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalianza kutolewa tangu siku ya Ijumaa huku matokeo kamili ya awali ya uchaguzi huo yakiwa yanatarajiwa kutolewa mnamo Desemba 31.

BY NEWS DESK