Watahiniwa 4 wa mtihani wa kitaifa kidato cha nne KCSE hawatapata matokeo yao baada ya kufutiliwa mbali na Baraza la Mtihani nchini, KNEC.
KNEC imewanyima matokeo yao watahiniwa hao kufuatia kuhusika kwao na udanganyifu wakati wa mtihani.
Akiongea mnamo Jumatatu wakati wa kutangaza matokeo ya KCSE mwaka 2023 katika shule ya Wasichana ya Moi huko Eldoret kaunti ya Uasin Gishu Waziri wa elimu Ezekiel Machogu amesema kulikuwa na visa vya watahiniwa 4,113 waliojuhusisha na udanganyifu katika mtihani huo.
Machogu alisema katika watahiniwa hao matokeo ya watahiniwa wengine 4,109 yamezuiliwa kwa siku 20 zaidi kwa uchunguzi kutokana na kushukiwa au kudaiwa kuhusika na udanganyifu.
“Kulikuwa na jumla ya watahiniwa 4,113 waliojihusisha na visa vya udanganyifu na katika hao tumefutilia mbali matokeo ya watahiniwa 4, na hao wengine waliosalia ambao ni 4,109 tumezuia matokeo yao kupisha uchunguzi kuhusiana na madai ya kuhusika na udanganyifu,” alisema.
Wakati uo huo watu 120 wakiwemo walimu wanaoaminika kusaidiana na wanafunzi kushiriki udanganyifu wanatarajiwa kushtakiwa.
Waziri Machogu aidha amebaini kuwa watu ambao watakosa kuridhishwa na suala lolote kuhusiana na matokeo hayo watatakiwa kuwasilisha malalamishi yao kwa jopo la kitaifa lililobuniwa na wizara ya Elimu kuangazia masuala yanayohusishwa na hitilafu katika matokeo ya mtihani.