Kitengo cha Kenya Hajj chini ya Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (SUPKEM) pamoja na Ufalme wa Saudi Arabia ulitia saini itifaki za msimu wa Hija wa 2024 huko Jeddah Januari 7, 2024.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Naibu wa Waziri wa Masuala ya Hijja na Umra kwa niaba ya Ufalme wa Saudi Arabia na Al-Hajj Hassan Ole Naado kutoka kitengo cha Hajj nchini Kenya.
Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Kenya MHE. Khalid A. Al-Salman na Dk Badr Al-Solami, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Hajj na Masuala ya Umra walikuwa miongoni mwa washiriki wakuu waliohudhuria sherehe hiyo iliyofanyika kaatika hoteli ya Assila, Jeddah.
Ujumbe wa Kenya Uliongozwa na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya ambaye pia ni Rais wa Kitengo cha Hajj nchini Kenya Al-Hajj Hassan Ole Naado, Katibu Mkuu Haji Abdullahi Salat, Naibu Mwenyekiti Shariff Muhudhar Khitamy, Katibu Mwenezi, Sheikh. Juma Musa Asmani na Mratibu wa Kanda ya Kaskazini Mashariki (Dk) Adan Yunis Sheikh Ibrahim ambao pia ni wajumbe wa suala zima la Hijja.
Makubaliano kati ya Wizara ya Hijja na Masuala ya Umra ya Ufalme wa Saudi Arabia na kitengo cha Hajj Kenya chini ya mwamvuli wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya yanabainisha ahadi na wajibu wa wahusika katika mapatano hayo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Masuala ya Hijja na Umra Mheshimiwa Dk Abdul Fattah Suliman Al-Mashat alisisitiza umuhimu wa kuzingatia muda uliowekwa katika maandalizi ya msimu wa hijja 2024. Waziri huyo alisisitiza kuwa Ufalme wa Saudi Arabia una nia kubwa ya kuhakikisha kwamba mahujaji kutoka pande zote za dunia wanapata huduma nzuri za kuwawezesha kutekeleza ibada zao za hijja bila tashwishi.
Kwa upande wake Ole Naado, alitoa pongezi kwa Msimamizi wa Misikiti Miwili Mitakatifu na kiongozi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mtukufu Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud na Mrithi wa Kifalme na Waziri Mkuu wa Ufalme wa Saudi Arabia Mtukufu Mohamed bin Salman kwa ahadi na juhudi zao za kuhakikisha kwamba mahujaji kutoka kote ulimwenguni ikiwemo Kenya wanaweza kutekeleza wajibu wao wa kidini kwa urahisi.
Ole Naado, alimhakikishia waziri huyo ushirikiano kamilifu kwa niaba ya jamii ya Waislamu katika Jamhuri ya Kenya. Alithibitisha kuwa Wakenya 4500 watahiji mwaka wa 2024 na wamejitolea kufuata kalenda ya matukio kama inavyoshirikiwa na Wizara ya Hajj na Masuala ya Umra ya Ufalme wa Saudi Arabia.
Ole Naado na wajumbe wenza kutoka kitengo cha Hajj nchini Kenya hata hivyo, watahudhuria Kongamano litakalofanyika juma zima la Hajj 2024 huko Jeddah, Saudi Arabia lililoitishwa na Wizara ya Masuala ya Hijja na Umra kuhudhuriwa na mwakilishi wa nchi 129 kuanzia Jumatatu 08/02/ 2024.