HabariNews

Idara Ya usalama Chonjo Kuzuia Uhalifu Kaunti Ya Mombasa

Idara ya usalama kaunti ya mombasa imesema imezidisha jitihada za kupambana na uhalifu eneo hilo ili kuwalinda wakaazi dhidi ya maovu yanayowakodolea macho.

Kwa muda sasa kaunti ya mombasa imekuwa ikionyesha mabadiliko makubwa ya kiusalama ikilinganisha na miaka kadhaa iliyopita.

Katika mahojiano ya kipekee na Sauti ya Pwani kamanda wa polisi kaunti hiyo Stephen Matu amesema hatua hiyo ni kutokana na ushirikiano mzuri baina ya taasisi za kiusalama na jamii eneo hilo.

Matu ameeleza jinsi wakaazi wamekuwa mstari wa mbele kuripoti visa vya utovu wa usalama katika vijiji vyao huku akiwahimiza wanajamii kuzidisha juhudi zao katika kupambana na visa vya uhalifu kaunti hiyo.

Kadhalika amefichua kuwa tayari maafisa wa usalama wamewakamata watu 5 wanaodaiwa kutekeleza uhalifu kutumia pikipiki ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakaazi kwa muda sasa.

Aidha amewataka wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma kuajiri dereva na makanga mahususi ili kuepuka kujipata katika mikono hatari ya kisheria pindi uhalifu utakapotekelezwa katika harakati ya

kuendeleza shughuli zao na kurahisishia idara ya usalama kuwatia mbaroni wahalifu wanaotekeleza visa hivyo katika usafiri wa aina hiyo.

Kamanda huyo wa polisi amewataka wakaazi wa kaunti hiyo kuchukua tahadhari mwafaka wakati wa kuabiri magari ya usafiri wa umma na katika kuendeleza shughuli zao za kawaida ili kuepuka kuporwa mali na kujeruhiwa na wahalifu.

Pia amesikitishwa na suala la watu kutaka kujitoa uhai katika kivukio cha likoni ferry akitoa wito kwa wote wenye matatizo ya kiakili kutafuta usaidizi mwafaka ili kulinda maisha yao.

 

BY BEBI SHEMAWIA AND MEDZA MDOE