HabariNews

WANAFUNZI 341 WAPATA UFADHILI WA MASOMO KILIFI.

Wanafunzi 341 wanaojiunga na shule za upili kaunti ya Kilifi wamepata afueni ya kuendeleza masomo yao baada ya kupokea ufadhili wa masomo kutoka kwa wakfu wa Jomo Kenyatta.

Wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE mwaka jana wakitarajia kujiunga na shule za upili kuanzia tarehe 15 mwezi huu wa Januari, mashirika na wadau mbali mbali yamejitokeza kufanikisha shughuli za masomo kwa wanafunzi hao kwa kutoa ufadhili.

 

Kulingana na naibu kamishna eneo bunge la Kilifi kaskazini Samuel Mutisya, msimu huu unatarajiwa kuwa na shughuli nyingi kufuatia kukamilika kwa mfumo wa elimu wa 8-4-4 huku serikali ikiendeleza agizo la kuhakikisha kuwa asilimia mia ya wanafunzi wa shule za msingi wanajiunga na shule za upili.

 

Mutisya alieleza kufurahishwa na wadau kujitokeza ili kufadhili masomo huku akitoa wito kwa wafadhili zaidi kujitokeza ili kuwasaidia wanafunzi wanaotoka kwenye jamii zisizojiweza.

“Hili ndilo darasa la nane la mwisho kwenye mfumo huu wa elimu na kama serikali tutahakikisha kuwa kila mwanafunzi anajiunga na shule ya upili. Na ndio sababu unaona wadau wengi wamejitokeza kuhakikisha kuwa wanawasaidia wanafunzi kujiunga na shule za upili. JKF wamekuwa wakitoa ufadhili kwa muda mwingi lakini kwa wakati huu wameongeza ufadhili wao na hapa kaunti ya Kilifi wametoa ufadhili kwa wanafunzi 341.” alisema Mutisya.

Kwa upande wake Eliud Nyangweso mwakilishi wa wakfu wa Jomo Kenyatta alisema wakfu huo unalenga kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi elfu 11 kote nchini, ambapo wanafunzi hao watapata ufadhili kwa kipindi cha miaka minne cha masomo ya sekondari.

 

Vile vile alieleza kuwa mwaka huu wakfu wa JKF umetoa ufadhili wao kwa wanafunzi waliopata alama 280 na zaidi katika mtihani wa kitaifa wa KCPE.

“Wakati huu wakfu wa JKF ambao ni mpango wa serikali ya Kenya, mwaka huu pekee tunachukua wanafunzi elfu kumi na moja kote nchini Kenya pamoja na kambi za wakimbizi huu ni ufadhili wa asilimia mia kwasababu unasimamia elimu yote ya sekondari na huo ufadhili unasimamia karo za shule, pesa za kununulia vitu vya matumizi binafsi ya mwanafunzi, nauli pamoja na hela ziada za mwanafunzi.” alisema Nyangweso.

BY ERICKSON KADZEHA.