Watu 10 wameripotiwa kufa maji katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Kwale tangu mwaka 2024 kuanza.
Haya ni kwa mujibu wa Idara ya Usalama kaunti ya Kwale iliyofichua kuwa mvua kubwa zilizoshuhudiwa awali mwezi Disemba mwaka jana huwenda zikawa sababu yake.
Kulingana na Kamanda wa polisi kaunti hiyo Steven Ng’etich visa hivyo vimekithiri katika maeneo ya fuo za bahari, mabwawa na hata katika vidimbwi vya maji ya kuogelea.
Ng’etich aliwataka wakaazi na wageni walioko katika kaunti ya Kwale kuwa makini na usalama wao wanapotembea kwenye fuo za bahari kuogelea.
“ Kuna visima vya maji ambavyo viko vijijini tunapata ripoti kwamba kwa namna moja au nyingine watu wamekufa maji. Mito vile vile watoto wakienda kuogelea tunapata ripoti kuna mtoto mmoja au wawili ambao labda wamekufa maji, kwahio hizo ripoti tukonazo na zinachunguzwa.” Alisema
Ng’etich hata hivyo aliwahakikishia wakaazi wa Kwale usalama wa kutosha ili kuona kuwa wakaazi wanatekeza shughuli zao za kiuchumi katika mazingira salama kwa maafisa wao kushika doria mara kwa mara.