Huenda nchi ikatumbukia katika mzozo mkubwa wa katiba na kupelekea ghasia na machafuko iwapo utawala wa Kenya Kwanza utazidi kupuza maagizo ya mahakama.
Ni kauli yake Jaji Mkuu nchini Martha Koome, akiuonya uongozi wa Kenya Kwanza dhidi ya kuishambulia idara ya mahakama.
Akihutubia mkutano wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Tume ya Huduma za Mahakama JSC, rais huyo wa mahakama ya Upeo ameukashifu utawala wa rais William Ruto kwa kupuuza maagizo ya idara ya mahakama na kuendelea kuishambulia idara hiyo licha ya kuwa huru kisheria.
Koome amesema kuwa utawala wa rais Ruto kwa sasa unaliweka taifa hili katika hali ya ghasia na machafuko kwa mfumo usiozingatia sheria.
Amebaini kutamaushwa na semi za viongozi wakuu serikalini ambao wameendelea kuashiria wazi na hata kutishia kuwa hatatii sheria na maagizo ya mahakama.
Ameonya kuwa iwapo uongozi wa Serikali ya Kenya Kwanza utakiuka maagizo ya mahakama basi taifa hili litakuwa pabaya zaidi na kutumbukia katika mgogoro wa kikatiba.
Itakumbukwa kuwa miongoni mwa maagizo ya mahakama yaliyoibua hasira za rais Ruto ni pamoja na kusimamishwa utekelezwaji wa mpango mpya wa Bima ya Afya ya Jamii, kuzuia utekelezaji wa sheria ya ushuru wa nyumba, kubinafsishwa kwa mashirika 11 ya serikali, na ubinafsishwaji wa bandari ya Mombasa na Lamu miongoni mwa miradi mingine ambayo serikali ilinuia kutekeleza.