Gavana wa Kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime amewataka wakaazi wa kaunti hiyo kuwa na subira anapojitahidi kuboresha uchumi Taita Taveta ambao amedai ulikuwa umedorora kiasa cha kikubwa kabla ya kuingia kwake ofisini.
Akizungumza katika hafla ya kutoa ufadhili kwa watoto 100 wanaojiunga na Kidato cha Kwanza kutoka familia zisizojiweza, gavana huyo alikiri kuwa alikumbana na changamoto nyingi katika serikali aliyorithi kutoka kwa mtangulizi wake Granton Samboja.
Kulingana na Mwandime alipata deni la Sh1.4 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na wakandarasi ambalo angali analilipia.
Hata hivyo,gavana huyo alisema kuwa serikali yake inajitahidi kuboresha huduma za afya, madini, elimu, kilimo, miundombinu na maendeleo ya jamii licha ya kuwa fedha wanazopata kutoka kwa serikali kuu ni chache mno na haziwezi kutekeleza maendeleo katika kaunti hiyo kikamilifu.
Mwadime alifafanua kuwa kati ya Sh400 milioni wanazopata kila mwezi, Sh320 milioni hulipa mishahara ya wafanyakazi, Sh20 milioni hununua madawa huku zilizosalia zikitumiwa kwa matumizi mbalimbali ya serikali.