HabariNews

ODM yalilia Donge katika Mgao wa Fedha Kukidhi Mahitaji yake.

Chama cha ODM kimelalamikia kupunguzwa kwa mgao na kucheleweshwa kwa fedha za chama hicho na serikali licha ya Afisi ya Usajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kutangaza kiwango cha pesa ambacho chama hicho kinafaa kupata.

Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alidai kuwa kati ya Sh308 milioni ambazo zilitengwa na afisi hiyo, chama cha ODM kimepokea Sh50 milioni pekee kufikia Januari 19, hali inayowaathiri sana utendakazi wa chama hicho kifedha.

Sifuna alifichua kuwa chama hicho kimekuwa kikikabiliwa na matatizo mengi ya kifedha, hasa kwenye ulipaji wa kodi ya afisi zake na uendeshaji wa shughuli za kuwasajili wanachama wapya.

Kulingana na Seneta huyo wa Nairobi, kwenye makadirio ya kwanza ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa serikali wa 2023/2024, vyama vya kisiasa vilikuwa vitengewe jumla ya Sh6 bilioni, lakini serikali ikapunguza fedha hizo hadi Sh1.6 bilioni.

Katibu huyo alifichua kuwa Kimsingi chama cha ODM hupata jumla ya Sh877 milioni, lakini fedha hizo zilipunguzwa hadi Sh308 milioni pekee akiongeza  serikali bado inakazia fedha hizo hata baada ya kuzipunguza.

Itakumbukwa kuwa kwenye mgao mpya wa fedha hizo chama tawala cha UDA ndicho kilipata mgao mkubwa baada ya  kutengewa Sh576 milioni huku vyama vya Jubilee na Wiper vikitengewa Sh135 milioni na Sh72 milioni mtawalia.

BY NEWS DESK