HabariLifestyleNews

Washukiwa 8 wa Ufisadi Bandarini Mombasa wafikishwa Kortini na Kuachiliwa kwa Dhamana

Maafisa 8 wa Halmashauri ya Bandari nchini, KPA waliokamatwa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC kwa madai ya kuhusika na ufisadi wa zaidi ya milioni 62 wamefikishwa mahakamani Mombasa kujibu mashtaka.

Washukiwa hao wameshtakiwa kwa kuhusika na ulaghai na kughushi stakabadhi za kandarasi za biashara katika zabuni bandarini humo.

Washukiwa hao Wanane hao ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Ugavi, KPA Yobesh Oyaro, Robert Bosuben, Rose Cherotich, Azenath Mageto, David Angwenyi, Norah Mugambi, Athanase Wambari, na Idd Arube

Hata hivyo mbele ya Jaji Alex Ithuku washukiwa hao wamekana madai hayo na kuachiliwa kwa bondi ama dhamana ya pesa taslimu kama ifuatavyo:

Robert Bosuben, Rose Cherotich, Azenath Mageto wameachiliwa kwa bondi ya shilingi 2,000,000 ama dhamana ya pesa taslimu shilingi 500,000 huku Idd Arube Nanyang ameachiliwa kwa bondi ya shilingi milioni 2 ama dhamana ya pesa taslimu 500,000.

Yobesh Oyaro, David Angwenyi, Norah Mugambi na Athanase Wambari wameachiliwa kwa bondi ya shilingi 1,000,000 ama dhamana ya shilingi laki moja pesa taslimu.

EACC ilikuwa inatarajia washukiwa 9 japo mmoja kwa jina David Arika alimaliza muda wake wa kudumu na hivyo mahakama imempendekeza kesi yake kushughulikiwa na mamlaka ya Bandari KPA.

Kesi hiyo sasa itatajwa tena mahakamani Mombasa mnamo Februari 7, 2024.

BY MEDZA MDOE