Afisa mmoja wa Serikali huko Ganze kaunti Kilifi amekamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC kwa madai ya wizi wa chakula cha msaada.
Teddy Buya Bonaya ambaye ni Msaidizi wa Kamishna wa GatuzI dogo la Ganze anatuhumiwa kuuza chakula hicho cha msaada ambacho kilifaa kusambazwa kaunti ya Tana River.
Kulingana na Msemaji wa EACC Erick Ngumbi, Bonaya anatuhumiwa kuuza chakula hicho chenye thamani ya shilingi 550,000 ambacho kilistahiki kusambazwa kwa wakazi wa eneo la Tana Kaskazini alikokuwa akihudumu awali.
Kwa mujibu wa EACC, Bonaya anadaiwa kutekeleza wizi wa magunia 300 ya chakula cha msaada ambapo mshukiwa huyo alitekeleza hayo mwaka 2020 alipokuwa naibu kamishna wa kaunti ya Tana River.
“EACC imemkamata afisa huyu anayesemekana kuhusika na wizi na uuzaji wa chakula cha msaada ambacho ni cha thamani ya zaidi ya nusu milioni na makosa haya yalitendeka mwaka wa 2020 wakati alikuwa anafanya kazi kama msaidizi wa Kamishna kule Tana River upande wa Tana North.” Alisema.
EACC imefichua kuwa Tume hiyo ilipokea madai ya afisa huyo kuhusika na ufisadi kwa kuuza chakula hicho mnamo Aprili 2020 na baada kukamilisha uchunguzi waliwasilisha faili yake kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Umma ODPP ambayo ilitoa idhini ya kukamatwa kwake.
“Tulipata idhini ya Mkrugenzi wa mashataka DPP afisa huyu akamatwe na kumshtaki kwa mashtaka ya kutumia ofisi vibaya inayohusiana na kuuza chakula cha msaada ambacho kilinuiwa kuwasaidia maskini kaunti ya Tana River,” alisema.
Afisa huyo alikamatwa siku ya Jumatano mjini Malindi na kupelekwa kituo cha polisi cha Garissa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Garissa mnamo Alhamisi Februari Mosi kufunguliwa mashtaka.
BY MJOMBA RASHID