Kwa mara nyingine tena Rais William Ruto amebaini kuwa hakuna litakalositisha juhudi zake za kuendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba za makazi ya bei nafuu.
Akiwa katika ziara huko eneo la Kanduyi kaunti ya Bungoma Rais amewakashifu wale wanaoelekea mahakamani kuusimamisha mradi huo akiwataja kuwa maadui wa maendeleo.
Rais Ruto amesema mradi huo na ule wa afya kwa wote utaendelea licha ya uamuzi wa mahakama kusitisha kukatwa kwa ushuru wa nyumba kutoka kwa wakenya walioajiriwa, huku akiwaonya wanakandarasi dhidi ya kusitisha mradi huo wa nyumba za bei nafuu.
“Nimeona jana ama juzi wanakandarasi wengine wameanza kuambia watu sijui maneno gani iko kortini, nataka niwambie vijana wakenya wanaofanya kazi katika mpango ya housing waendelee, contractors waendelee kazini kwa sababu hakuna vile tunaweza kutoa mtu kazini, watu elfu 130 mimi nitawapeleka wapi? Si waendelee kufanya kazi,” alisema.
Kiongozi huyo wa nchi amesema kuwa wakenya walimpa idhini ya kuendeleza mradi huo kwa kuwa unabuni nafasi za ajira hasa kwa vijana nchini akiwataka wanakandarasi hawapaswi kuwafukuza wafanyakazi kwa namna yoyote ile kwani kazi sharti iendelee.
“Kwanza nataka nisukume kufika mwisho wa mwaka huu vijana nusu milioni watakuwa wanafanya kazi katika mpango ya housing kila mtu anaweka pesa kwa mfuko anaenda kulisha familia yake,” alisema.
BY MJOMBA RASHID