HabariNewsSiasa

Raila Apuuzilia Mbali Uamuzi wa Mahakama kuamuru IEBC Kuundwa Upya Kabla ya Ripoti ya NADCO

Kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga amepuuzilia mbali uamuzi wa Mahakama kuu ulioagiza mchakato wa kuunda upya Tume ya Uchaguzi IEBC uendelee pasi mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) yaliyowaslishwa bungeni.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara huko Kamukunji Odinga aliutaja uamuzi wa Jaji Mugure Thande uliotolewa Alhamisi wiki iliyopita kutokuwa na msingi kwani kamati ya awali ya IEBC ilikuwa imevunjwa na bunge.

Mahakama ilikuwa imeamuru jopo lililoteuliwa, kuanza mchakato wa kuwateua makamishna wa tume hiyo ya uchaguzi mara moja.

Odinga aliipuuzilia mbali, akisisitiza kuwa kuundwa kwa Tume mpya ya IEBC kutafanyika punde tu baada ya Bunge kupitisha ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya mazungumzo.

“Juzi mahakama moja inasema eti kamati ya mbele ya kuteua wanachama wa IEBC ati iendelee na kazi yake, nasema hiyo ni upuuzi. Hiyo kamati haiwezi kufanya kazi maana tayari ilivunjwa na bunge. Sasa ile ripoti ya kina Wandayi na Kalonzo ikienda mbele ya bunge ipitishwe ndio tutaanza mambo ya IEBC,” alisema.

Haya yamejiri katika mkutano wa chama cha ODM wa kuendeleza zoezi la kusajili wanachama wake huku shinikizo la kumtaka kinara huyo kuwa debeni mwaka 2027 likiendelea kutolewa na viongozi.

Wandani wa Odinga wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir na aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliff Oparanya waliendelea kushinikiza kinara wao kuwa debeni huku wakifichua kuwa Odinga atakuwa debeni katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Nataka sauti ya Kamukunji isikike hadi Mombasa, wangapi wanakubaliana na mimi ya kuwa Baba Raila Amollo Odinga ni lazima awe kwenye debe mwaka 2027?” Aliuliza Gavana Nassir huku wafuasi wakishangilia.

“Mkijisajili kama ODM hii mambo ya kuwa tumetenga, eti tumeweka itakuwa imekwisha 2027 ili Raila Odinga aingie state house,” alisema Oparanya.

Shinikizo hili linajiri licha ya Kinara huyo wa mrengo wa Azimio akionekana kukwepa siasa hizo za mapema japo akisema kuwa muda sahihi ukifika atajizungumzia mwenyewe.

BY MJOMBA RASHID