HabariNewsSiasa

Wetangula Hafai kuwa Spika! Raila Odinga Amkashifu Spika Kwenda Kortini

Spika wa bunge Moses Wetangula hafai kuwa spika wa bunge la Kitaifa nchini kutokana na kukiuka sheria za utendakazi wake.

Ni kauli yake kinara wa Upinzani Raila Odinga ambaye amebaini kuwa hatua ya Spika huyo kuwasilisha kesi mahakamani kupinga uamuzi wa mahakama uliositisha utekelezaji wa sheria ya ushuru wa nyumba inamuondoa kuwa Spika wa bunge.

Akizungumza Jumapili katika mkutano wa kusajili wanachama wa ODM huko Kamukunji jijini Nairobi, Odinga alisema Spika wa bunge hana mamlaka ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga uamuzi wa sheria ambayo ilipitishwa na bunge na kutiwa sahihi na rais Ruto.

“Bwana Spika Wetangula mweneyewe ameenda mahakamani hii sheria ilikwua imetoka kwa bunge ikaenda kwa Bw. Ruto akaweka sahihi sasa watu wengine wakenda mahakamani, mahakama ikasema hiyo sheria si halali. Bwana spika katika ulimwengu mzima hana uwezo kuenda mahakamani anaenda kama nani? Bwana Wetangula hafai kuwa Spika wa bunge la Kenya.” Alisema.

Kulingana na Odinga Spika ni mtumishi wa bunge na hakupaswa kuwasilisha kesi mahakamani pasi idhini ya wabunge wa bunge la kitaifa akisisitiza kitendawili cha suala la sheria ya ushuru wa nyumba kilipaswa kuachiwa serikali kuu na idara ya mahamaka.

“Kama wewe ni Spika umeshapitisha sheria kazi yako imekwisha hapo sasa imebaki kati ya serikali kuu na mahakama, sio kazi ya bunge tena. Wewe huwezi Kwenda mahakama bila kuuliza wabunge, spik ani mtumishi wa wabunge huezi kuenda mahakama bila idhini ya wabunge, alienda kama nani?” aliuliza Odinga, huku umati ukimshangilia.

Wakati uo huo kinara huyo wa ODM aliendelea kukashifu mkutano wa rais Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome uliofanyika mwezi jana akidai kuwa mkutano huo ulikuwa ishara tosha kuwa Idara ya Mahakama imetekwa nyara na Serikali Kuu hasa baada ya kuahidiwa kuongezewa mgao wa fedha na kuajiriwa majaji zaidi.

“Ruto alisema yeye ati hajali mambo ya mahakama akaalika yule mama Chief Justice. Nilimshauri huyo mama (Koome) asiende ikulu utashikwa mateka huko, akaenda kutoka huko akasema eti amepewa pesa ya kuajiri majaji…ni makosa sana”

Amesema kikao cha bajeti na nyongeza ya fedha kwa idara ya mahakama hakikupaswa kufanyika katika Ikulu bali kupitia kuwasilisha maombi Bungeni ili kujadili na kupitisha ombi lao, akimtaka Jaji Mkuu Koome kufuata mkondo sahihi wala si kupitia vikao vya Ikulu ya rais.

“Mambo ya pesa kama mahakama inataka pesa haifanywi ikulu. Nimeambia huyo mama ya kwamba kama mahakama inataka pesa unafanya ombi kwa bunge sio Ikulu, hiyo ni makosa makubwa sana.” Alisema.

BY MJOMBA RASHID