HabariNews

Afueni! Huduma za Afya Mashinani Kuimarika Zaidi Kaunti ya Kwale

Huduma za afya zinatarajiwa kuimarika zaidi huko Mwakijembe wadi ya Ndavaya eneobunge la Kinango kufuatia ufunguzi wa zahanati.

 Wakazi wa eneo hilo sasa watapata afueni ya kusafiri mwendo mrefu kusaka matibabu baada ya Serikali ya kaunti ya Kwale kuwakabidhi rasmi kituo hicho cha afya eneo hilo.

Wakizungumza na wanahabari wakazi hao wakiongozwa na Menza Rocha hawakuficha furaha yao wakisema zahanati hiyo itawapunguzia mahangaiko hususan akina mama wajawazito waliokuwa wakilazimika kutembea mwendo mrefu wa zaidi ya saa mbili kutafuta huduma za afya.

“Tulikuwa tukimaliza masaa mawili kufikia huduma za afya Mkang’ombe mama akitoka asubuhi ni arudi jioni, sasa tunashukuru tumeletewa zahanati hapa Mwakijembe,” alisema mkaazi mmoja.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa zahanati hiyo huko eneo la Mwakijembe, Gavana wa Kaunti hiyo Fatuma Achani amewahakikishia wakazi huduma bora za afya kuimarishwa zaidi hasa mashinani kwa kuongeza wahudumu zaidi wa afya katika zahanati na vituo vya afya sawia na upatikanaji wa dawa na vifaa vya matibabu.

“Ni kweli zahanati hii ilikuwa inahitajika sana. Siku moja tu imefunguliwa tayari  mhudumu amehudumia zaidi ya watu 600. Tukishirikiana na mjumbe wenu tumeweka vifaa vya kisasa na dawa zipo na tayari tumeandikisha na KEMSA tutakuwa tunapata supply direct hadi hapa Mwakijembe na maeneo mengi ya nchi.” Alisema Achani

Zahanahati hiyo ya Mwakijembe inaongeza idadi ya vituo vya afya katika maeneo mbalimbali kaunti hiyo kufikia 165.

BY BINTIKHAMIS KADIDE