HabariNews

Waziri Mutua: Jiunge na NYS kwanza au Usahau Kujiunga na Idara ya Jeshi au Polisi!

Idadi ndogo ya vijana imejitokeza kushiriki zoezi la usajili wa vijana kujiunga na huduma ya vijana kwa taifa NYS mjini Kilifi.

Katika shughuli iliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Utalii na Wanyamapori nchini Dkt. Alfred Mutua ili kusajili makurutu hao kujiunga na NYS ni msichana mmoja pekee aliyejitokeza katika wadi ya Sokoni eneo bunge la Kilifi kaskazini kushiriki zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Waziri Mutua aliyeanzisha rasmi zoezi hilo amesema, idadi ndogo ya vijana waliojitokeza kwenye zoezi hilo inatokana na wengi kukosa ufahamu wa kutosha kuhusu umuhimu wa NYS.

Aidha amewahimiza wasichana kujitokeza na kushiriki sajili hizo hata ikiwa wamejifungua, ili waweze kupanga vyema maisha yao ya baadae.

“Pia tumeona upungufu wa wasichana katika usajili huu wa makurutu wa NYS. Haijalishi hata kama wewe umejifungua mtoto, kuzaa si kos ahata kama umezaa mtoto muachee nyumbani kisha wewe njoo usajiliwe uendelee. Wengine labda walipata watoto wakiwa wadogo Kijana aliyekuzalisha yeye yuko sawa anakimbiakimbia huko wewe njoo ujitengezee maisha yako,” alisema.

Mutua amewahimiza vijana wazidi kujitokeza kwenye sajili za NYS huku aksistiza kuwa asilimia 95 ya vijana wanaofanikiwa kufuzu watapewa kipaumbele kujiunga na vikosi vya usalama pamoja na jeshi la ulinzi nchini.

Katika zoezi la leo idadi ya vijana wanaotarajiwa kuchukuliwa ni 25, ambapo 15 kati yao ni wavulana na 10 wakiwa wasichana.

“Nafikiri vijana hawajaelewa maana ya NYS. Wengi ya wanaoingia jeshi walipitia NYS, sasa watu hawajafahamu hayo, wanadhani sio kazi wanakaa nyumbabni ati wanangoja siku ya usajili wa jeshi ama polisi, nasema ng’o! Kuja NYS kwanza upande ngazi kama hujakuja NYS basi sahau mambo ya jeshi,” alisema Waziri Mutua.

Zoezi sambamba na hilo lilifanyika Jumatano Februari 7 katika eneo bunge la Kaloleni.

Ikumbukwe kuwa Waziri wa masuala ya Utumishi wa Umma alichapisha idadi ya vijana waliopangwa kusajiliwa katika kile wadi ambapo katika wadi ya Sokoni kaunti ya Kilifi vijana 16 walipangwa kusajiliwa na vijana 10 kutoka wadi ya Tezo.

BY ERICKSON KADZEHA