HabariNewsSiasa

Kalonzo Atishia Kufanyika Maandamano Nchini Iwapo Jaji Mkuu Koome Atabanduliwa

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ametishia kuwa kutakuwa maandamano kote nchini iwapo mapendekezo ya kumng’atua uongozini Jaji Mkuu Matha Koome yatafanikiwa.

Akizungumza katika ibada ya Jumapili eneo bunge la Tigania Mashariki kaunti ya Meru, Kalonzo alisema hatua hiyo ambayo inalenga kumuondoa madarakani jaji mkuu ni njama ya kuhujumu na kuingilia utendakazi wa idara ya mahakama nchini.

Aidha Kalonzo alibaini kuwa bunge la kitaifa kwa sasa limemezwa na Serikali kuu na halina uhuru wa kufanya uamuzi wowote hasa kuhusu miswada na ajenda za serikali.

“Tutaandamana kutoka Maua, Seikuru, Meru na kote huko. Hatutaruhusu hilo, na huwezi kufanya hivyo (kumbandua Jaji Mkuu). Hiyo ndiyo ngome ya mwisho ya uhuru wetu,” alisema Kalonzo.

Kalonzo amewataka wabunge ambao wangali kuunga mkono muungano wa Azimio kuhakikisha wanapinga kila pendekezo ambalo linaenda kinyume cha matakwa ya Wakenya.

Ombi la kuondolewa uongozini Jaji Mkuu Martha koome liliwasilishwa na Mkenya Michael Kojo Otieno ambaye alidai kuwa Koome hakufuata utaratibu wa kisheria unaofaa kuteua wanachama wa Bodi ya kusikiliza rufaa ya kesi kuhusu Ushuru.

Kojo alidai kuwa Jaji Mkuu hakuwa na uwazi na utendakazi, akiongeza kuwa alifanya ubaguzi dhidi ya watu waliotuma maombi ya kuwa wanachama wa bodi hiyo.

“Hatua ya Jaji Mkuu kuteua wanachama zaidi ya idadi iliyohitaji ilikiuka kipengee cha 4b cha Sheria ya Mahakama ya Rufaa ya Kodi,” ilisema sehemu ya Kesi iliyowasilishwa.

BY MAHMOUD MWANDUKA