HabariLifestyleMichezoNews

Walimu wa Sekondari Kilifi waacha Chaki na Kusakata Soka

Timu ya walimu wa shule za upili kutoka eneo la Chonyi kaunti ya Kilifi imewakosea wenyeji wao Tezo Veterans adabu kwa kuwalambisha sakafu kwenye mchezo wa kirafiki uliojaa mbwe mbwe na mahanjam ya kila aina mjini Tezo.

Ngarambe hiyo iliyohusisha timu ya kabumbu ya walimu wa shule za upili kutoka eneo la Chonyi maarufu kikosi kazi imeonyesha umahiri ugenini kwa kupata ushindi wa mabao 3-2.

Kulingana na nahodha wa kikosi kazi Rodgers Ondiek, walimu wenzake waliamua kuungana na kusakata kabumbu kama njia ya kutafuta suluhu ya changamoto ya kuandikishwa kwa matokeo duni katika mitihani ya kitaifa kaunti ya Kilifi.

Kwa upande wake Mike Baya nahodha wa Tezo Veterans alieleza kufurahishwa na hali ya mchezo huku akiwapongeza wapinzani wao kwa kuonyesha ubabe kwenye ngarambe hiyo.

Mwakilishi wa gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro kwenye ngarambe hiyo Teddy Yawa ambae ni katibu wa idara ya Kilimo, aliwazawidi washindi shilingi elfu 10 pesa taslimu huku Tezo Veterans wakipokezwa kitita cha shilingi elfu 5.

By Erickson Kadzeha