HabariLifestyleNews

Mkuu wa Hazina ya Fedha Kaunti ya Kwale Akamatwa Tena baada ya Kuachiliwa

Makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC wamemkamata tena Mkuu wa Hazina ya Fedha Kaunti ya Kwale baada ya kuachiliwa kwa dhamana na mahakama ya Mombasa.

Vincet Chirima Mbito, ametiwa mbaroni na maafisa hao akihusishwa na kesi ya ufisadi inayoendelea na inayohusisha upataji kwa njia ya ulaghai shilingi milioni 3 milioni kutoka kwa hazina ya kitengo kilichogatuliwa.

Afisa huyo Mkuu amekamatwa na maafisa hao wa EACC na amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Bandarini huku msako kwa sasa ukiendelezwa kuwasaka maafisa wengine wawili wa kaunti waliotambulika kama watu wanaohusika na kesi hiyo.

Chirima ambaye awali alikuwa amekamatwa na ndugu zake wanne alikuwa amefikisha mahakamani Mombasa na kushtakiwa kwa kuilaghai kaunti ya Kwale shilingi milioni 22 kabla ya kuachiliwa kwa dhamana.

Washukiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Alex Ithuku mnamo Jumanne mchana, wakikabiliwa na mashtaka 5 yanayohusiana na ulaghai, ambapo wamedaiwa kushawishi kutolewa kwa zabuni 10 kwa kampuni zao mbili.

Washirika wake Chrima ni Mongo Mbito Mongo anayehudumu kama Afisa wa Ushuru wa Kaunti hiyo, Hassan Shilingi Mbito dereva anayehusishwa na Kampuni ya Maji safi na Maji taka ya Kwale, Mwaiwe Mongo Mbito anayehudumu kama Afisa Ununuzi kaunti ya Kwale na Chindoro Mongo Mbito anayehudumu katika Wizara ya Afya kwa sasa.

“Washukiwa walitekeleza makosa hayo kati ya Juni 2018 na Julai 2021 ndani ya Kaunti ya Kwale nchini Kenya,” ilisema taarifa ya ODPP.

Hata hivyo washukiwa hao walikana mashtaka hayo wakisema hawana hatia na kupewa dhamana ya shilingi milioni 1 kila mmoja na mdhamini mmoja na dhamana mbadala ya pesa taslim shilingi 500,000.

Kesi yao imepangwa kusikilizwa mnamo Machi 12, 2024.

BY MJOMBA RASHID