Vijana kote nchini wamehimzwa kujiepusha na visa vya ufisadi ili kuboresha maisha yao na maisha ya jamii.
Naibu kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa, Owen Baya amesema ni jukumu la vijana kuhakikisha kuwa wanaungana na idara husika za kukabiliana na ufisadi kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
Baya aliyepia mbunge wa Kilifi Kaskazini ameongeza kuwa ufisadi umeathiri maendeleo kote nchini katika huku akisistiza kuwa ili kuboresha kizazi kijacho vijana lazima wajumuishwe katika vita hivyo dhidi ya ufisadi.
“Ikiwa huwezi kuwekeza na kuhimiza taifa kuzingatia uadilifu mtu wa kwanza kuathirika ni vijana. Unapoangalia wanapotafuta kazi na kuhangaishwa wengi wanaoathirika zaidi ni hawa vijana, hivyo lazima nao wajitokeze kukemea.” Alisema.
Wakati uo huo Baya alitoa changamoto kwa Tume ya Maadili na kukabiliana na ufisadi nchini EACC kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake ipasavyo n ahata kuwajumuisha vijana katika vita hivyo.
“Taasisi tulizo nazo hazifanyi vyema kwa kuendeleza ufisadi. Lazima tuilinde nchi yetu kwa kukabiliana na ufisadi nchi iwe salama,” alisema.
BY ERICKSON KADZEHA