HabariKimataifaLifestyleMombasaNews

Rais Ruto aashiria Makubaliano ya Kuwa na Mgombea Mwenza wa Kike katika Kura za Urais Zijazo

Rais William Ruto amebaini kuwa atasalia kujitolea kuhakikisha kuwa sheria ya thuluthi mbili ya jinsia imetekelezwa kikamilifu katika chama chake cha UDA na ndani ya serikali ya Kenya Kwanza kwa jumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Kimkakati wa G7 la Magavana Wanawake nchini, huko jijini Nairobi, rais amesema serikali yake imefuata mikakati Madhubuti ili kutimiza kiwango hitajika cha Katiba kuhusu ujumuishaji wa Kijinsia na itakuwa mstari wa mbele kudhihirisha ahadi yake hiyo.

Rais Ruto ameahidi kulishinikiza bunge kuhakikisha linapitisha mswada wa thuluthi mbili wa usawa wa jinsia ili kuhakikisha kuwepo kwa usawa bungeni sawia na kuchangia idara tofauti za kiserikali kuongeza idadi ya wanawake katika kulitumikia taifa.

“Wakati huu tutahakikisha kuwa sheria ya thuluthi mbili ya usawa wa jinsia inafanikiwa. Na shughulio inayoendelea bungeni na ripoti ya NADCO sasa ikijumuisha yale waziri Jumwa na wenzake wamepigania. Najua kuna mahesabu mengi lakini katika mswada huu utakaofika bungeni tutahakikisha kuwa inapitishwa na kuwepo na uongozi wa wanawake bungeni,” alisema.

Kufuatia hayo rais amemtwika jukumu Mwenyekiti wa chama cha UDA aliyepia Gavana wa Embu Cecily Mbarire kuunda msururu wa sheria ambazo zitahitaji mgombea urais wa kiume kuwa na mgombea mwenza wa kike na kinyume chake.

Rais aidha amedokeza kuwa wamekubaliana yeye na naibu wake Rigathi Gachagua jinsi mambo yatakavyoelekea siku za usoni na kwamba muda sahihi ukifika sharti wataafikia uamuzi wa pendekezo la kuwa na mgombea mwenza wa urais mwanamke.

“Rigy G (Rigathi Gachagua) na mimi tukifika hapo mbele na tumepangana tumekubaliana vile itaenda, lazima tukubaliane kuendelea mbele ikiwa mgombea wa urais ni mwanamume katika chama chetu mgombea mwenza lazima awe mwanamke, na ikiwa mwanamke ni mgombea urais basi mwanamume awe mgombea mwenza,” alisema rais.

Rais alieleza matumaini yake kuwa vinara wengine wa vyama vya kisiasa watakubaliana na pendekezo hilo ili kuafikia kikamilifu sheria ya thuluthi mbili za jinsia, sheria ambayo pia itatekelezwa kwa uwanaiaji wadhfa wa Ugavana.

Kiongozi huyo wa taifa alisema suala la jinsia kuhitaji ujasiri na uungwaji mkono ili kukubalika na jamii zote, hata hivyo alisifia juhudi na utendakazi wa magavana wanawake nchini akisema kuwa uwajibikaji wao ni kampeini mwafaka ya kubadili msimamo wa jamii katika kuchagua wanawake wengi katika chaguzi zijazo.

“Suala la jinsia linahitaji ujasiri na kuungwa mkono ili likubalike na jamii zote, lakini niseme pia juhudi za magavana hawa wanawake uwajibikaji wenu ni kampeini tosha kubadili mtazamo wa jamii, na wengi watachagua viongozi wanawake mbeleni,” alisema.

Uzinduzi wa mkakati wa G7 wa Muungano wa Magavana wanawake mnamo Alhamisi, unajiri huku Taifa likijiandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake hapo siku ya Ijumaa Machi 8 2024.

 

BY MJOMBA RASHID