Mwenyekiti wa muungano wa mataifa ya Caribbean, Irfaan Ali ametangaza kujiuzulu kwa waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry.
Haya yanajiri kufuatia viongozi wa Kanda hiyo kukutana huko nchini Jamaica kabla ya kuafikiana Waziri Mkuu huyo kuachia ngazi za uongozi kutokana na ongezeko la ghasia hasa katika mji mkuu wa Port au Prince na kote nchini humo kwa jumla.
Irfaan aliye pia rais wa Guyana, amesema wanatambua kujiuzulu kwake baada ya kuanzishwa kwa baraza la mpito wa urais
Tangazo hilo la kujiuzulu limetolewa huku rais huyo kwa sasa akiwa amekwama huko Porto Rico kutokana na magenge ya uhalifu kulemaza shughuli mbalimbali na kuzidisha wimbi la ghasia na machafuko yaliyomzuia kurudi nyumbani.
Ariel Henry ambaye hakuchaguliwa na aliyeshikia mamlaka tangu mwaka 2021 ameshindwa kurejea nchini mwake tangu alipofanya ziara nchini Kenya wiki mbili zilizopita kutia saini mkataba wa kuruhusu taifa hili kutuma maofisa wa polisi nchini humo kurejesha utulivu na usalama.
“Safari hii kwa sasa ni dharura na inahitajia haraka, ikiwa kile tulichokiona kule Port au Prince ni suala la kufuatilia basi inaashiria udharura wa misheni hii,” alisema Rais Ruto.
Henry aakizungumza katia Ikulu ya Nairobi alizidi kutoa wito kwa mataifa na vikosi vilivyojitokeza kupambana na magenge kushirikiana na taifa lake hilo.
“Bidhaa haziwezi kuingizwa wala kutoka ndani ya Haiti na tulitoa ombi hili na rais ukajitokeza ukasema mnataka kusaidia kusimama na sisi kwa umoja, nakushukura sana Rais,” alisema Ariel.
Haya yanajiri siku moja baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Prof. Kithure Kindiki mnamo siku ya Jumatatu kubaini kuwa Kenya haitalegeza msimamo wake wa mpango wa kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti ili kusaidia kurejesha usalama nchini humo.
“Kwa sasa tuko katika hatua ya maandalizi ya kuwapeleka maafisa wetu wa polisi huko, mipango yote iko sawa ikiwemo ya hali ya mikataba ya makubaliano ya vikosi na sheria za kuzuia na kukamata kwa washukiwa iko chonjo na vikosi vya Kenya vitakuwa sehemu ya misheni ya kimataifa ya usalama wa Haiti,” alisema.
Alikuwa akizungumza mnamo Jumatatu huko kaunti ya Machakos.
Waziri Kindiki aliweka wazi kuwa lengo la kutuma maafisa limekamilika na hivi karibuni maafisa hao watajiunga na vikosi vingine vya usalama kuyakabilia magenge hayo yaliyolemaza shughuli katika taifa hilo.
BY MJOMBA RASHID