Mbunge wa Nyali Mohammed Ali amewataka viongozi wa kidini kuwajibika na maswala yanowahusu badala ya kuingilia mambo yasiyo na msingi.
Akionekana kuwajibu viongozi wa kidini wa Baraza la SUPKEM na CIPK walioibua maswali kuhusu ugavi wa chakula cha msaada katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, Ali amesema kuwa rais Ruto alimtuma kugawa chakula hicho kutokana na kuwa kiongozi pekee anayeegemea mrengo wa serikali.
Mbunge huyo aidha alisema chakula hicho kikiwa cha serikali ya kitaifa hakitapitia kwingineko na kwamba msaada wowote kutoka serikali kuu atausimamia na kuhakikisha unawafikia walengwa wote kaunti ya Mombasa.
“Nilisikia Supkem na viongozi wengine wakilalamika kuhusu hii chakula… Mimi nimetumwa na Rais niwafikishie na kwa kuwa mimi ndiye mbunge pekee wa UDA hapa nawakilisha serikali na nitazunguka Mombasa nzima nihakikishe akina mama zetu mnapata.
Wakati uo huo Ali, aliwataka viongozi hao Kuwajibika na mambo yanayowakabili wananchi kama vile maswala ya dini, dawa za kulevya, ufisadi, na tabia potovu zinazojitokeza kwa vijana wa mkoa wa pwani.
“Tunawaambia SUPKEM washughulikie inayowahusu mambo ya dini, wasaidie kupiga vita ufisadi, mambo ya mihadarati, wizi na mambo ya kukemea ushoga na usagaji watusaidie huko waache siasa.” Alisema.
Haya yanajiri siku kadhaa baada ya viongozi wa kidini kutoka Baraza Kuu la waislamu nchini SUPKEM na wenzao kutoka Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, kuibua maswali tata kuhusu usimamizi na utaratibu wa ugavi wa chakula hicho cha msaada.
Viongozi hao walidai kwamba huenda chakula hicho kikakosa kufikia walengwa na hata kugawanywa kisiasa kufuatia hatua ya serikali kukikabidhi Mbunge huyo wa Nyali na seneta maalum Miraji Abdillahi licha ya kila mwaka kukabidhiwa viongozi wa kidini kusimamia shughuli hiyo.
BY MJOMBA RASHID