HabariNews

Polisi Wanasa Washukiwa 10 wa Genge la Uhalifu Kisauni, Msako Ukiendelea

Idara ya polisi kaunti ya Mombasa inaendeleza msako wa genge la wahalifu lililovamia wakazi katika mtaa wa Toa Tugawe-Mshomoroni eneo bunge la Kisauni.

Genge hilo la wahalifu takribani 30 linalodaiwa kujihami kwa mapanga na silaha nyingine butu limekuwa likihangaisha wakazi wa maeneo ya Toa TugaweKadongo na maeneo mengine.

Tayari maafisa wa polisi wamewanasa washukiwa 10 wanaodaiwa kutekeleza uvamizi wa duka moja na kupora wenyeji mtaani Toa Tugawe kabla ya kumjeruhi mmiliki wa duka hilo.

Kulingana na maafisa wa polisi baadhi ya mali na bidhaa zilizoporwa zilipatikana kutoka kwa washukiwa hao pamoja na vifaa vinavyoaminika kutekeleza uhalifu huo ikiwemo mapanga.

Hata hivyo polisi wanasema kwamba uchunguzi unaendelezwa ili kuwakamata washukiwa zaidi wanaokisiwa kuhusika kwenye kisa hicho.

Alice Kirote mmiliki wa duka ambaye alivamiwa nyumbani kwake nusura kuuawa, kwa sasa anaendelea kuuguza majeraha mabaya hospitalini, majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa na genge hilo usiku wa Jumanne wiki hii.

Walinivamia wakitaka niwatolee pesa nikawaambia sina nimefanyia biashara, ndio wakanipiga kichwani nilipowaangalia wakanipiga tena nikapiga nduru, walipoona kutajaa watu kwa kelele hiyo wakanipiga panga linguine kwa kichwa na kuwasha kiberiti akarusha moto na wakanenda.” Alisema.

Kufuatia hayo Viongozi sasa wanashinikiza idara za usalama kuwajibika vilivyo kupambana na makundi ya uhalifu yanayotishia usalama wa wakazi wa Kisauni.

Rashid Juma Bedzimba Mbunge wa Kisauni ametaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya genge linalodaiwa kuhangaisha wakazi.

Mbunge huyo aidha ametaka uchunguzi kufanyika nah atua kuchukuliwa kwa wazazi wa kijana wa umri wa miaka 17 aliyekamtwa akiwa na baadhi ya mali yaliyoibwa na silaha butu walizotumia.

BY NEWS DESK