Shirika la Msalaba Mwekundu limefanikiwa kuwaokoa abiria waliokuwa wamekwama barabarani katika Kijiji cha Tulla kaunti ya Tana River.
Katika taarifa waliochapisha kwenye akaunti yake ya X Shirika hilo limesema abiria wote 51 waliokuwa wamekwama ndani ya basi hilo wameokolewa huku kipaombele kikipewa akina mama, watoto na wale waliokuwa wagonjwa.
Basi hilo lililokuwa likisafiri kutoka Wajir kuelekea Nairobi lilisombwa na maji katika eneo hilo la Tulla mapema alfajiri ya Jumanne Aprili 9 na kuacha abiria wakihangaika kwa muda mrefu huku juhudi za kuwaokoa awali zikigonga mwamba.
Shirika hilo aidha limesema linashughulikia kuwaokoa abiria wengine waliokwama barabarani kufuatia kukatika kwa Barabara eneo la Tulla katika kaunti hiyo.
Haya yanajiri huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga nchini, MET imetangaza kuwa sehemu nyingi za nchi zitaendelea kurekodi mvua kubwa wiki hii.
Kulingana na ilani ya hivi punde zaidi ya Idara hiyo mvua itaendelea kunyesha kote nchini katika nyanda za Pwani, eneo la kati, Bonde la Ufa, nyanda za Kusini Mashariki, Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi mwa Kenya.
MET pia imesema baadhi ya kaunti hasa zile za Kaskazini Mashariki zitarekodi viwango vya juu vya joto zinazozidi nyuzi joto 30.
Haya yanajiri huku abiria kadhaa wakikwama barabarani na kulazimika kukesha usiku kucha wa kuamkia leo juu ya basi walilokuwA wakisafiria kusombwa na maji.
Dereva wa basi hilo lililokuwa likitokea Nairobi kuelekea Wajir alilikumbana na maji ya mafuriko ya Mto Tana yaliyofunika Barabara hiyo.
Tukio hilo linajiri kufuatia taarifa ya tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu nchini, KenHA iliyotangazia umma kufungwa kwa Barabara Kuu ya Nairobi-Garissa kutokana na mafuriko eneo la Mororo lililoko kati ya Madogo na Daraja la Tana River.
KENHA ilisema mafuriko hayo ni kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji kutoka Mto Tana.
BY MJOMBA RASHID