HabariNews

Kenya Airways Yafutilia mbali Safari zake za Ndege za Dubai Kufuatia Hali ya Anga

Shirika la ndege la Kenya Airways limesitisha safari yake ya Kwenda na kutoka Dubai kutokana na hali mbaya ya hewa na mafuriko yanayoendelea katika Milki ya Falme za Kiarabu (UAE).

Kwenye taarifa yake ya Jumatano, KQ imesema kuwa safari nyingine ya ndege yake ilisitishwa mnamo Jumanne Aprili 16 kutokana na hali mbaya ya anga iliyogubika mataifa ya Mashariki ya Kati kufuatia mvua kubwa.

KQ imesema mafuriko kutokana na mvua kubwa yamesababisha changamoto za utendakazi, na kupelekea kusitishwa kwa safari hizo.

Shirika la Ndege la Kenya Airways limewashauri wateja walioathirika kuwasiliana kwa namabari +24 711 024 747, WhatsApp: +254 705 474 747, au barua pepe: customer relations@kenya-airways.com.

Mnamo siku ya Jumanne, mvua kubwa kupita kiwango cha kile kinachoshuhudiwa kwa mwaka ilinyesha kwa siku hiyo na kupelekea mafuriko katika Uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi wa Dubai huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki.

Hali hiyo ilipelekea kusitishwa kwa muda wa dakika 25 huduma zote na zaidi ya safari 50 za ndege zikifutiliwa mbali.

Mvua kubwa kupita kiasi iliyopelekea mafuriko ilishuhudiwa katika mataifa ya Qatar, Bahrain, Saudi Arabia na Oman na kupelekea vifo vya watu 18.

BY MJOMBA RASHID