AfyaHabariLifestyleNews

Madaktari Kubaini Msimamo wao Kuhusu Kusitisha Mgomo au La

Muungano wa madaktari nchini KMPDU hii leo unatarajiwa kutoa msimamo wao wa iwapo watasitisha mgomo wao au la.

Hii ni baada ya upande wa serikali kuwapa madaktari muda wa ziada hadi hii leo kuhitimisha majadiliano yao na kutoa mwelekeo wa mgomo unaoendelea.

Baada ya kuwasubiri kwa siku nzima viongozi wa muungano wa Madaktari kutia saini makubaliano ya kurejea kazini hapo jana, viongozi wa madaktari hawakutokea katika Jumba la Mikutano la KICC.

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei awali akieleza kuwa Serikali ipo tayari kwani mazungumzo ambayo wamekuwa wakiyafanya tayari yamefikia asilimia 96 ya matokeo yanayotarajiwa.

Koskei anasema licha ya wajumbe wa madaktari kujikokota, kanuni za kurejea kazini kwa madaktari ziliandaliwa na wawakilishi wa pande zote mbili na upande wa Serikali umekubali utiaji saini kufanyika leo.

Mgomo wa madaktari umeingia siku 40, tangu Machi 14 madaktari waliposusia kazi, na wamekuwa wakiandamana kulalamikia serikali kushindwa kuwaajiri madaktari wanagenzi sawia na kushindwa kutekeleza Mkataba wa Makubaliano (CBA) 2017.

Hata hivyo licha ya serikali kuwapa ofa ya kuwalipa madaktari wanagenzi shilingi 70,000 pekee kinyume na shilingi 206,000 wanazoshinikiza, madaktari waliikataa ofa hiyo.

BY MJOMBA RASHID