HabariNews

Wazazi Kaunti ya Kilifi waililia Serikali Kumrejesha shuleni mwanafunzi wa sekondari aliyeolewa.

Kina mama wachanga kaunti ya Kilifi wamepata matumaini mapya ya kuendelea na masomo kufuatia shirika la kijamii la MAPENZI CHARITY CBO kuanzisha mpango wa kuwatafutia ufadhili wa kuendeleza masomo yao.

Wengi wa akina mama hao sasa wanaonekana kuwa na ari ya kutaka kubadili hali zao za kimaisha kwa kuendeleza elimu ama kupata ujuzi.

Kaunti ya Kilifi ikiwa miongoni mwa kaunti zinazoorodheshwa kuwa na visa vingi vya mimba za utotoni, kina mama hao wachanga huenda wakapata nafasi nyingine ya kutimiza ndoto zao maishani kwa kuendelea na masomo.

Kulingana na Chantel Mapenzi Kaingu mwanaharakati wa kupambana na ugomvi wa jinsia na aliyepia mwasisi wa shirika la MAPENZI CHARITY CBO mjini Kilifi, ndoto za kina mama wengi wachanga zimekatishwa kutokana na dhana potofu katika jamii kuwa wasichana wanaojifungua hawafai kurudi shuleni hali inayowafanya kina mama hao kuwa na maisha magumu.

Anasema kufikia sasa zaidi ya kina mama wachanga 20 wamenufaika na mpango huo huku akieleza kuwa wanalenga kusaidia kina mama wengi zaidi kaunti ya Kilifi.

Aidha ametoa wito kwa wahisani pamoja na serikali ya kaunti kuwasaidia kupata raslimali za kuendeleza mpango huo akieleza kuwa uhitaji uliopo ni mkubwa ila changamoto hiyo huenda ikalemaza juhudi zao.

BY ERICKSON KADZEHA