Wabunge wameeleza kughadhabishwa na hatua ya Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kukaidi mwaliko wa kuhudhuria kikao kilichoitishwa na kamati ya bunge kuhusu utekelezwaji wa katiba.
Wakihutubia waandishi wa habari hapa mjini Mombasa mnamo Ijumaa Aprili 26, wabunge hao wamekashifu hatua ya Koome kususia mwaliko wao na hata kushindwa kutuma manaibu wake wawili kumwakilisha katika kikao hicho licha kutuma udhuru wa kutohudhuria.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Gathoni Wamuchomba, Wabunge wamesema walikuwa wamemwalika Koome kuja kujibu tuhuma na malalamishi yaliyowasilishwa kuhusu hujuma za afisi yake dhidi ya utendakazi wa Tume ya Huduma za Polisi (NPSC), zikiwemo kutumia mamlaka yake vibaya na kunyanyasa maafisa wengine wa polisi.
“Yale mambo yamezuka hapa ni ya kushangaza sana, kwamba makamishna wa hiyo Tume wameondolewa walinda usalama wao, wamenyanyaswa na kufungiwa ofisi wasihudhurie mikutano na IG, hawana mahali ya kutafuta haki yao, inakuwa kazi ya kusajili makurutu wa polisi nchini ni kazi ya IG peke yake na hiyo sio vile Katiba imeelekeza.
Inspekta Jenerali wa Polisi Bwana Koome yuko nje ya mwongozo, amekiuka sheria na amekataa kujitetea kwa huu mkutano tumekuwa nao hapa.” Alisema Wamuchomba.
Wamuchomba ambaye pia Mbunge wa Githunguri amesema Koome amekuwa akifanya kazi kidikteta kwa kutozingatia sheria wala kukaa kushirikiana na makamishna wa tume ya Huduma za Polisi kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maafisa wa polisi.
“Huyu IG Koome amekuwa mtu wa kifua hataki kuingia kwa mikutano kujadiliana hayo maneno yote, anachukua hayo yote anasema ni kazi yake na si kazi yake. Na anatumia katiba vibaya kunyanyasa wanachama wa Tume hiyo ya Kitaifa ya Huduma za Polisi.” Alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji aliye mwanachama wa kamati hiyo amesema kutokana na uchunguzi wao Koome anahujumu utendakazi wa Tume ya huduma za polisi hasa baada ya kukosa kuhudhuria kikao hicho.
“Kile kwa hakika kinachotokea wakati Huduma ya Polisi inataka kutekeleza jukumu lake, tumeona ni kuhujumu idadi hitajika ya kufanya mikutano ya Kipengee cha 2 Cha sheria ya Polisi, na nataka kukashifu bvikali suala kwamba IG Koome ni mtu wa hujuma, ndio maana amehepa kikao hiki na hakutuma mwakilishi licha ya kuwa na manaibu wawili,” alisema.
Mbunge huyo alihusisha matatizo ya ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo nchini ni kutokana na utepetevu, hujuma za ndani ya tume hiyo na ukosefu wa muafaka wa mashauri baina ya Inspekta Jenerali na makamishna wanaofuatilia mienendo ya tume.
“Ni lazima kuwe na Tume ya Huduma za Polisi na ofisi iliyo huru kwasa tunajaribu kuhusisha kinachotokea kwa idara zetu za usalama na kukosekana usalama kwa baadhi ya maeneo ya taifa hili na suala la hujuma kwa kweli na kuifanya Afisi ya IG kuwa ya kibinafsi.” Alisema Mukunji.
Wabunge hao sasa wamempa ilani Koome kuitikia wito wa kuhudhuria kikao ili kujibu tetesi zinazomkabili mbele ya kamati hiyo la sivyo kamati itashinikiza kubanduliwa kwake mamlakani mara moja, kwa kile walichokisema ni kutozingatia sheria.
“Tunatoa ilani kwa IG, kama hatatii kuja kujibu maswali, kama hatarekebisha sisi kama Kamati tuna nguvu kutoka Katiba na tunapendekeza yeye afutwe kazi, ang’olewe kwa mamlaka yake. Alisema.
“Naunga mkono Mwenyekiti wetu na ninakashifu vikali, na tutachukua hatua ikihusu kumwita IG aje ajieleze mwenyewe kuhusu malalamishi haya na kama hatatii kuitikia wito wetu tena tutasonga mbele kupendekeza atolewe ofisini akiendelea kuhujumu utendakazi wa Tume ya Huduma za Polisi.” Alisema Mbunge Mukunji
Haya yanajiri huku wabunge wa Kamati hiyo ya masuala ya Utekelezwaji wa Katiba wakikutana kwa siku 2 hapa mjini Mombasa, baada ya kufanya vikao sawia hapo awali jijini Nairobi.
BY MJOMBA RASHID