Taifa la Kenya limeahidi kuunga mkono azma ya Baraza Jipya la Mpito la Rais nchini Haiti lililoapishwa katika harakati zake za kulikomboa na kuliongoza taifa hilo lililotawaliwa na magenge yenye silaha.
Katika taarifa yake kwenye mtando wa X, Rais William Ruto amepongeza mabadiliko ya uongozi na kuyataja mabadiliko hayo kuwa hatua muhimu katika mpito wa kisiasa wa Haiti.
Rais Ruto amesema Baraza hilo la Mpito lina jukumu la pekee la kusonga mbele kwa haraka ili kuanzisha tena Idara muhimu za Serikali zilizo muhimu sana katika kurejesha sheria na utulivu mwafaka kwa kuleta matumaini kwa Wahaiti wote.
“Kenya inahakikishia TPC ya Haiti uungaji mkono kikamilifu katika kuongoza taifa hilo kujikomboa katika hali iliyoko sasa.” Alisema.
Baraza hilo la Mpito la Rais lenye wanachama 9 llilichukua uongozi rasmi hapo jana Alhamisi baada ya kuapishwa kwake na hivyo kurasimisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Ariel Henry.
Katika Baraza hilo, Michel Patrick Boisvert aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa fedha wa Waziri Mkuu Henry sasa atakuwa Kaimu Waziri Mkuu hadi pale Baraza hilo la Mpito litakapochagua Kiongozi mpya, kuunda baraza la mawaziri na kuunda baraza la uchaguzi linalopania kufanikisha uchaguzi ujao wa taifa hilo wa mwaka 2026.
Itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Wahaiti walipopiga kura ilikuwa katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka 2016.
BY MJOMBA RASHID