HabariLifestyleMazingiraNews

Serikali Yatangaza Ijumaa Siku ya Mapumziko ya Kitaifa Kuwaenzi Wahanga wa Mafuriko

Serikali imetangaza siku ya Ijumaa Mei 10, wiki hii kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Upanzi wa Miti.

Akizungumza kwenye kikao kaunti ta Kajiado rais amesema siku hiyo ambayo itakuwa Mei 10 aidha itatumika kukumbuka maisha ya Wakenya walioathirika na walioaga dunia kutokana na mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika Rais amedokeza kuwa siku hiyo pia imetengwa kwa ajili ya zoezi la upanzi wa miti ikiwa njia moja wapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mapema leo Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura aliandika kwenye akaunti ya X kuwa; “Notisi ya Gazeti rasmi la serikali itatolewa kwa athari hii. Waziri wa Mazingira, Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi, Soipan Tuya atahutubia waandishi wahabari leo kutoa maelekezo zaidi.”

Katika taarifa ya hivi punde ya serikali kuhusu athari ya mafuriko kote nchini msemaji wa serikali amesema kwamba kufikia sasa takriban watu 75 kote nchini hawajulikani waliko, huku watu 238 wakiwa wameaga dunia kutokana na mafuriko yanayoshuhudiwa nchini.

BY MAHMOUD MWANDUKA