HabariNews

Wauguzi Wengi Wahamia Nchi Za Ng’ambo Kufanya Kazi Ili Kupata Ujira Mzuri

Wauguzi humu nchini wakiadhimisha wiki ya wauguzi, imebainika kuwa wauguzi wengi wenye tajriba kubwa kazini wanasusia kazi na kuhamia nchi za ng’ambo kufanya kazi ili kupata mishahara mizuri.

Kulingana na mshirikishi wa afya ya uzazi kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti, taifa hili linapoteza kwa kiwango kikubwa ubora wa huduma za afya kwa kile anachodai kuwa wauguzi kuhamia nchi za ng’ambo kufanya kazi.

Amesema mazingira magumu ya kufanyia kazi, ukosefu wa nyongeza ya mishahara pamoja na marupurupu ni baadhi ya hoja zinazowafanya wengi kususia kazi humu nchini, hali anayodai imeleta changamoto katika utoaji wa huduma katika idara hiyo ya afya.

“Lile ambalo limefanyika tangu mwaka 2017 mpaka sasa wauguzi wengi ambao walikuwa na tajriba ya haiba ya juu wamesafiri kuelekea mataifa ya Marekani au Uingereza ama Canada kwa hivyo tunapoteza sana. Na wito wangu kwa serikali nikuwa kama taifa la Kenya tunapoteza na hatutaweza kurudisha tena. Kwa hivyo swala la mishahara ni swala muhimu sana kwa wauguzi lakini jambo hili limewekwa chini sana.” alisema Miriti.

Kwa upande wake mwenyekiti wa muungano wa wauguzi nchini tawi la Kilifi, Nyevu Juliana ameitaka serikali kutekeleza makubaliano yaliyoafikiwa kati ya viongozi wa muungano wa wauguzi na serikali ya kuwaongezea mishahara pamoja na marupurupu mengine, ili kuwatia motisha zaidi wauguzi katika utendakazi wao.

“Katika halmashauri ya serikali ya kaunti ya huduma kwa umma tumeweza kuwa na mazungumzo kuhusu mkataba wa makubaliano ya mwaka 2017 ambayo inatuelekeza ni mambo gani ambayo tunataka tukafanyiwe nyongeza katika huduma zetu.

“Kwa hivyo katika hayo makbaliano tumeangazia vitu vitatu ambapo kuna swala la sare ambalo mwajiri wetu anatupa marupurupu ya shilingi 20,000 kila mwaka, lakini tunaomba iongezwe hadi shilingi 25,000 na swala la pili ni marupurupu ya kufanya kazi katika hatari ambapo tunapewa chini ya shilingi 5,000 ambayo tunataka iongezwe ili kutoa motisha kwa wauguzi.” alisema Nyevu.

Jesca Deche ambaye ni msimamizi wa kitengo cha afya ya familia katika hospitali ya rufaa kaunti ya Kilifi ameeleza kuwa ukosefu wa wauguzi wa kutosha kumetatiza utoaji wa huduma hasa kwa wanawake wajawazito, ambapo tajriba huhitajika katika kutoa huduma.

Aidha amesema mfumo wa kuwaajiri wauguzi haujakuwa wakufurahisha kutokana na wauguzi kupewa ajira kwa mikataba.

“Katika ujira tumekaa muda mrefu karibu miaka mitano sasa hatujaajiri wauguzi na wako katika muda huo wameenda nyumbani (kustaafu) ama wameenda nchi za ng’ambo kutafuta ujira mzuri na jambo hili limeathiri hasa katika huduma za wauguzi kutoka kwa zahanati mpaka kwa hospitali kubwa.

“Na hasa wakati huu tumefika kiwango cha kwamba utakuta hospitali kubwa wachukue wauguzi kwa mikataba ama ajira ya muda wa kuhesabu tu ambapo wale ambao wanatajriba wanaenda na wale wanakuja hawana watu wa kuwafunza ili kupata tajriba hitajika.” alisema Deche.

ERICKSON KADZEHA