HabariLifestyleNewsTravel

Serikali Kupanua huduma za Reli ya SGR kuunganisha Afrika Mashariki na Kati

Waziri wa uchukuzi nchini Kipchumba Murkomen ametoa wito kwa wahudumu na wafanyakazi wote katika shirika la reli nchini  kuboresha utoaji wa huduma katika shirika hilo ili kufanikisha shughuli za usafiri na miradi mingine katika sekta hiyo ya uchukuzi nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mipango na mikakati ya shirika hilo ya mwaka wa 2023-2027 iliyoandaliwa hapa mjini Mombasa, Murkomen alisisitiza haja ya viongozi na wahudumu wengine katika sekta za uchukuzi nchini kushirikiana ili kuafikia malengo ya maendeleo katika sekta hizo.

“Nina furaha kujua kwamba mipango iliyowekwa na shirika hili la reli ikiwemo ikiwemo  kupanua operesheni za Bandari ya Mombasa, kuboresha miundombinu ya reli, kuongeza kiwango cha mizigo inayosafirishwa kutoka 16% hadi 42%ifikiapo mwaka wa 2027 na pia kuongeza  malighafi na usimamizi wa shirika hilo kwa jumla. Mipamgo hii itakuwa na faida sio tu kwa shirika bali pia kwa taifa kwa jumla.”

Waziri huyo aidha alisema serikali inapania kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka mjini Naivasha hadi Kisumu mradi ambao pia unalenga kuunganisha Kenya na mataifa mengine ya Jumuiya ya muungano wa Afrika Mashariki.

“kama serikali tunalenga kuendeleza ujezni wa reliu ya kisasa kutoka naivasha hadi malaba. Haya ni kulingana na malengo ya serikali kupitia shirika hili ambapo serikali inalenga kuunganisha kenya pamoja na mataifa jirani. Hii itaboresha biashara pakubwa na kukuza uchumi wa taifa.”

Kwa upande katibu wa kudumu katika wizara ya uchukuzi Mohammed Daghar alisema kama serikali wanalenga kuimarisha huduma za reli ili kupunguza hasara ambayo shirika hilo limekuwa likikadiria ya zaidi ya shilingi bilioni mbili wakielenga kuafikia faida ya bilioni tisa kufikia mwaka wa 2027.

Katibu huyo aliongeza njia mojawapo ya kuafikia malengo hayo ni kupanua huduma za reli kote nchi akisema serikali imeweka mikakati ya kuanzisha miradi hiyo ili kuafikia mojawapo ya malengo ya ruwaza ya 2030.

“Kwa sasa shirika hili la ndege linakadiria hasara ya bilioni mbili ila tunalenga kuongeza faida ya kibishiara hadi bilioni tisa ifikiapo 2027. Hili litaafikiwa kwa kupanua miundombinu ya reli kwa kuendeleza ujenzi wa reli hadi maeneo tofauti nchini.”

Usimamizi wa shirika hilo ukiongozwa na mkurugenzi mkuu Philip Mainga ulisisitiza haja ya kuafikiwa kwa malengo ya shirika hilo ili kurahisha shughuli za usafiri nchini.

Kulingana naye, shirika hilo limepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za usafiri na kama viongozi wa shirika hilo wanalenga kuboresha sekta hiyo ya uchukuzi hata zaidi.

“Tumetathmini kwa kina mahali tumetoka kama shirika , mahali tulipo kwa sasa na kule tunalenga kufikia iwapo mikakati tunayoiweka tutaitekeleza kikamilifu. Hivi karibuni, tunaweka kiwango kipya cha hadhi katika usafiri wa reli, kiwango bora zaidi kuwahi kushuhudia katika historia ya usafiri wa reli nchini.”

Haya yanajiri huku serikali kuu ikilenga kuboresha miundombinu ya uchukuzi nchini kama vile angatua za ndege, barabara na miundombinu mingine hatua ambayo inalenga kuimarisha pakubwa usafiri na biashara nyinginezo nchini.

BY NEWS DESK