HabariNews

Kinaya cha SRC! Maseneta Wakataa Nyongeza ya Mishahara Wakidai Ugumu wa Uchumi

Maseneta sasa wamepinga nyongeza ya Mshahara waliyopewa na Tume ya Kutathmini Mishahara na Marupurupu ya wafanyakazi wa umma, SRC wakieleza haja ya kumpunguzia mzigo Mkenya mlipa ushuru.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amesisitiza haja wanasiasa kuhakikisha wanapunguza matumizi kwa kukata utumizi mbaya wa fedha wakati wa kutayarisha bajeti ya matumizi ya wabunge na maafisa wengine bungeni.

Tunapaswa kuangalia upya bajeti yetu katika bunge hili na tuone wapi tunaweza kukubaliana kwa pamoja kupunguza gharama na matumizi ili wananchi wahisi kuwa tunapunguza mzigo na sio kuwaongezewa wananchi wakatwa ushuru.

Kina kinapaswa kufanywa kunapotayarishwa bajeti na wafanyakazi wa bunge wawe wakweli na Wakenya, kuna njia za kupunguza matumizi, mfano kadi yangu ya malipo ya Expressway naipata ina shilingi 377,000 hata kama nitatumia barabara hiyo mwaka mzima sitawahi kutumia pesa yote hiyo. Binafsi sihitaji pesa hiyo.” Alisema.

Naye Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Seneti Aaron Cheruiyot amepinga nyongeza hiyo ya mshahara akisema kuwa  mapato yay a viongozi ni sharti yaende sawa na hali ya uchumi ilivyo kwa sasa.

Ameisuta SRC kwa nyongeza hiyo akiibua maswali ni kwanini Tume hiyo ilisalia kimya wakati wa maandamano ya kupinga serikali badala ya kutoa sulhu la kutatua changamoto za kiuchumi nchini.

Kwa upande wake Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema wabunge na maafisa wengine sarikalini hawafai kuongezewa hata shilingi wakati huu uchumi wa taifa ukiwa umedorora.

Ikumbukwe kuwa SRC mnamo siku ya Jumanne iliwapa nyongeza ya mishahara maafisa wakuu serikalini, wakiwemo rais na naibu wake, Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri, makatibu, Magavana, Wabunge na Maseneta na hata wawakilishi wadi.

Kulingana na SRC Wabunge na Maseneta sasa watapokea shilingi 739,600 kila mwisho wa mwezi, huku Maspika Moses Wetangula wa Bunge la Kitaifa na Amason Jeffa Kingi wa Seneti wakipewa nyongeza ya shilingi milioni 1.2 na marupurupu mengine.

BY MJOMBA RASHID