Timu ya Likoni 1 ndio watakaopeperusha bendera ya kaunti ya Mombasa katika mashindano ya Kabumbu kuwania ubingwa wa Dimba la Dola Intercounty Super Cup.
Hii ni baada ya timu hiyo kuilaza Likoni 2 mabao 6-5 kupitia mikwaju ya penalty, kwenye mchuano uliodhihirisha mbwembwe na kila pande kujihami vilivyo dhidi ya mashambulizi.
Kwenye finali hiyo ya Dola Super Cup, Makala ya Mombasa Edition iliyosakatwa mnamo Jumapili katika uga wa Mwahima huko eneobunge la Likoni, na kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki ashiki wa kabumbu, ilishuhudia timu zote mbili zikidhihirisha ubabe na soka la burudani ya hali ya juu.
Kwa dakika 90 za mchezo Debi hilo la Likoni lilibainisha ugumu na uhalisia wa jinsi ilivyo kwa mechi za debi baada ya sare ya 1-1 dakika 90 za mchezo, na ushindani mkali ukashuhudiwa katika upigaji penalti kila timu ikitia kimyani penalti zake 5 za kwanza.
Hata hivyo shujaa wa ngarambi hiyo alikuwa ni Kipa Likoni 1 aliyewanyima wapinzani ushindi baada ya kupangua penalty ya ziada ya Said Abdallah wa Likoni 2 huku kiungo matata wa Likoni 1 Marco Cena akiitumia nafasi hiyo kuweka mkwaju wake wavuni na kuipatia timu yake ushindi.
Sadam Suleiman mkuu wa kitengo cha mauzo katika kampuni ya Dola ambao ndio wadhamini wakuu wa michuano hiyo, amesema kuwa lengo lao la kutambua na kukuza vipaji katika kaunti ya Mombasa limefanikiwa huku akiwa na imani kuwa baadhi ya wachezaji wa michuano hiyo watachukuliwa kucheza katika baadhi ya timu katika ligi kuu na zile za madaraja ya juu kuendelea kukuza talanta zao.
“Lengo letu limefanikiwa pakubwa, tumeona vijana wa vipaji wakisakata mpira jamii na mashabiki wakijitokeza. Na tunao maskauti na mameneja hapa wanaofuatilia na tunatarajia baadhi ya wachezaji hapa watapata nafasi kuchukuliwa kuchezea klabu za ligi ya hapa na kimataifa,” alisema Sadam.
Sadam alisema kupitia wavuti na mtandao wao wanatoa fursa kwa vijana kutambulika kitaifa na kimataifa kwa kuonyesha vipaji vyao vya usakataji kabumbu, akifichua wanapania kuendeleza michuano hiyo kwa kaunti zote nchini punde watakapokamilisha Makala ya Ukanda wa Pwani.
“Tuna mtandao mkubwa unaofuatilia haya mtandao wa dolasupercup.com na tumeonseha wachezaji hawa wote na kwuapa nafasi kujulikana ulimwenguni tukikuza na kuonyesha vipaji vyao kwa kuwapa nafasi. Na baaa ya hapa ni Makala ya Pwani na tunapanga Kwenda kwa kaunti zote 47 nchini Kenya.” Alisema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Mombasa Football Association Goshi Juma Ally amewataka wadhamini nchini kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wanakuza vipaji vya vijana ili kukumbatia kandanda kama njia moja wapo ya kujipatia riziki.
“Lengo kubwa la michuano hii ni kuleta vijana pamoja na kukuza vipaji na kuweza kuwandaa kwa mechi kubwa kubwa na michuano ya ushindani zaidi. Mashabiki wanapenda mpira sana na umeona jinsi walivyojitokeza kwa wingi, kinachohitajika ni wadhamini wajitokeze zaidi wajitolee kuimairisha mchezo huu vijana wapate motisha na riziki ili tuwainue.” Alisema Goshi.
Wakati uo huo Goshi alieleza kuwepo haja ya kuimarishwa kwa viwanja na miundombinu yake ili kutoa nafasi ya vijana zaidi kukuza vipaji.
“Tukipata viwanja ama miundombinu ikiimarishwa sawa sawa bila shaka mambo yatakuwa bora zaidi na vipaji kuendelea.” Alikariri.
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir amewashkuru wadhamini wa michuano hiyo Dola kwa juhudi zao za kukuza talanta huku akiahidi kuimarisha hali ya viwanja katika kaunti ya Mombasa.
“Talent za vijana ni muhimu kuwaunga mkono kuja kwa shughuli kama hizi, na kampuni na wadhamini kama hawa ni vizuri zaidi.” Alisema.
Gavana Naasir aidha alisema wanafanya kila juhudi ili kumaliza kujenga uwanja wa manuspaa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kiwanja hicho kuchezewa AFCON.
“Kuhusu ule uwanja wetu mkubwa tuna mpangilio saa hii na tunazungumza na wale wadhamini kutusaidia kuweza kuilipia na baadaye sisi kama kaunti tuwalipe taratibu taratibu panapo majaliwa itumike, Mombasa iweze kuandaa mechi za AFCON.
Lakini kwanza viwanja vitakavyokuwa tayari ni Mwahima, Bomu na uwanja wa Mbuzi, ule wa Manispaa yab Mombasa ni mkubwa si rahisi vile lakini tuna imani.” Alisema.
Michuano ya Dola Super Cup inaendelezwa katika kaunti zote 6 za Pwani, na Likoni 1, Mshindi wa michuano ya Dola Makala ya Kaunti ya Mombasa alitia kibindoni shilingi laki 1.
Likoni 1 FC na sasa ataingia katika droo ya timu 8 bora kuwania ubingwa wa Pwani, ambapo Mshindi wa jumla wa michuano hiyo kote Pwani atatia kibindoni shilingi milioni 1.
BY MJOMBA RASHID