Magavana na manaibu wao wanaostaafu wamepata pigo baada ya Mahakam kuu kuamua kuwa maafisa hao wakuu katika serikali za kaunti hawana haki ya kupokea marupurupu au Pensheni iliyobainishwa kama vile maafisa wengine wa serikali wanaohudumu katika serikali ya kitaifa.
Uamuzi huo unajiri kufuatia kesi iliyowasilishwa na baraza la Magavana COG, dhidi ya tume ya kitaifa ya kuratibu marupurupu na mishahara nchini SRC iliyosikilizwa mnamo Julai 25 mwaka huu na Jaji Lorence Mugambi katika Mahakama ya Milimani.
Kulingana na kesi hiyo, baraza la magavana lilitaka magavana na manaibu wao pindi wanapostaafu wapate pensheni kama wanavyopata mafisa wengine wa serikali hasa serikali ya kitaifa.
Aidha SRC ilieleza kuwa iwapo mpango huo utaidhinishwa utakuwa na athari kubwa kwa maafisa wa serikali za kaunti na ile ya kitaifa na kuacha rasilimali kidogo kwa maendeleo ya kitaifa kwa manufaa ya wanachi katika utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa SRC, mpango huo vile vile utasababisha mzigo mzito kwa serikali zinazoingia na vile vile kwa vizazi wa kugahramia malipo hayo.
Ikumbukwe kuwa magavana na manaibu wao wanapokea chagua la malipo ya huduma baada ya kukamilisha hatamu zao za uongozi ambapo hupokea kitita cha asilimia 31 ya jumla ya mishahara yao ya kila mwaka waliohudumu.
BY MAHMOOD MWANDUKA